1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la Miaka 50 ya Umoja wa Ulaya

Mohamed Dahman23 Machi 2007

Azimio la Berlin kuadhimisha miaka 50 ya Umoja wa Ulaya hapo Jumapili litatowa wito kwa umoja huo kufanya mageuzi makubwa kwa miundo ya taasisi zake zinazochakaa kufikia mwaka 2009.

https://p.dw.com/p/CB57
Umoja wa Ulaya Miaka 50
Umoja wa Ulaya Miaka 50Picha: DW-TV

Sehemu ya rasimu ya azimio hilo imepatikana na shirika la habari la Uingereza Reuters.

Kansela Angela Merkel anataka azimio hilo lizinduliwe wakati wa shamra shamra zitakazohudhuriwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Berlin kuzinduwa harakati zake za kufufuwa katiba ya umoja huo ambayo imekwama tokea ilipokataliwa na wapiga kura nchini Ufaransa na Uholanzi hapo mwaka 2005.

Azimio hilo lenye kurasa zipatazo mbili halitaji juu ya katiba hiyo jambo lilikuwa likipingwa na baadhi ya serikali za Umoja wa Ulaya.

Rasimu ya azimio hilo lilioandikwa kwa jina sisi watu wa Ulaya linasema tumeungana kwa lengo la pamoja la kuupa nguvu msingi wa pamoja ambao umejenga Umoja wa Ulaya itakapofikia chaguzi za bunge la Umoja wa Ulaya hapo mwaka 2009.

Mwanadiplomasia mmoja amesema baadhi ya nchi hazikifurahia maneno yaliounda rasimu hiyo lakini hazitarajiwi kulipinga.

Amesema hawatotaka kuharibu sherehe ya kuzaliwa matukio yaliopangwa kufanyika katika bara lote la Ulaya kuadhimisha miaka 50 ya Mkataba wa Rome ambao ulianzisha Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya hapo tarehe 25 mwezi wa Machi mwaka 1957.

Masuala juu ya hatima ya maudhui ya rasimu hiyo yanaendelea kubakia ambayo itatiwa saini na Ujerumani kama Rais wa Umoja wa Ulaya,Halmashauri ya Umoja wa Ulaya na Bunge la Umoja wa Ulaya na sio nchi wanachama 26 zilizobakia.

Lakini Merkel analiona azimio hilo kama lenye kuunga mkono juhudi zake za mageuzi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumami Frank Walter Steinmeir ameliambia bunge la Ujerumani kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji misingi mipya na kwamba hilo linatakiwa lifanyike kwa njia ya katiba.

Waziri Mkuu wa Uholanzi Jan Peter Balkanende amesema watu wanaendelea kuwa na mashaka juu ya katiba hiyo ambayo ingeliweza kubadili mfumo mzima wa kupiga kura wa makao makuu ya Umoja wa Ulaya yalioko Brussels Ubelgiji pamoja na kuanzisha wadhifa wa kipindi kirefu wa urais na waziri wa mambo ya nje wa Umoja huo lakini hata hivyo amesema kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji mageuzi.

Amesema kila jengo linahitaji kufanyiwa matengenezo, kufanywa kuwa la kisasa ili kwenda na mahitaji ya nyakati za sasa jambo ambalo pia linahitajikwa kwa bunge la Umoja wa Ulaya.

Rasimu ya azimio hilo ambalo lugha yake inakusudia kuwa rahisi kufahamika na raia wa kawaida linapongeza neema za mataifa ya Ulaya.

Azimio linasema bara letu lilikuwa limeteketezwa na vita, uchumi wake ulikuwa umeanguka na lilikuwa limegawika kwa misingi ya itikadi.Muungano wa Ulaya umetuleteya amani na ustawi wa uchumi.

Linaongeza kusema ni kwa kuwa pamoja tu tunaweza kulinda mfumo wa kupigiwa mfano wa jamii ya Ulaya katika kipindi cha usoni. Soko la pamoja na sarafu ya euro imetufanya kuwa na guvu zaidi kuweza kujenga mahusiano ya kiuchumi na ushindani kwa mujibu wa maadili yetu.

Jamhuri ya Czeck,Poland,Uingereza,Uholanzi na Ufaransa zinategemewa kuwa nchi ngumu kwa Merkel kuweza kuzishawishi wakati akishinikiza mipango yake kuweka ramani mahsusi juu ya katiba ya Umoja wa Ulaya.