1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la Baraza la Usalama juu ya Darfur

1 Agosti 2007

Baraza la Usalama la Umoja Mataifa limepitisha kwa kauli moja hatua ya kupeleka majeshi katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan.

https://p.dw.com/p/CB2I
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Ban Ki moon amesema hatua hiyo ni ya kihistoria ambapo wanajeshi na polisi alfu 26 wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika watapelekwa katika jimbo hilo ili kulinda amani.Amesema hatua hiyo ni ishara thabiti kwamba jumuiya ya kimataifa inadhamiria kuwasaidia watu wa Darfur.

Jeshi hilo litachukua mahala pa askari alfu 7 wa Umoja wa Afrika waliokuwa wanakabiliwa na uhaba wa vifaa.Jukumu la askari hao linawaruhusu kutumia nguvu endapo itakuwa lazima.

Akizungumzia juu ya azimio la Baraza la Usalama waziri mkuu wa Uingereza bwana Gordon Brown amesema anatumai kwamba serikali ya Sudan itaanza kuchua hatua.

Sudan imekaribisha azimio hilo.Balozi wa nchi hiyo nchini Uingereza ameeleza hayo. Balozi huyo bwana Omer Sidding amesema azimio hilo ni hatua inayoelekea kwenye lengo sahihi.

Serikali ya Sudan ilifikia mapatano na wawakilishi wa waasi wa Darfur juu ya kusimamisha mapigano.Mapatano hayo yalitiwa saini nchini Nigeria mwaka jana lakini makundi mengine ya waasi hayakutia saini mapatano hayo.

Tokea mgogoro wa Darfur ufumuke miaka miine iliyopita watu zaidi wasiopungua laki mbili wameshakufa kutokana na mapambano baina ya makundi ya waasi na wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali ya Sudan.Watu wengine zaidi ya milioni 2 wamegeuka wakimbizi.

AM