1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yaitimua Madagascar.

20 Machi 2009

Andry Rajoelina, kiongozi mpya wa Madagascar, leo ameamkia kibarua kigumu. Umoja wa Afrika, AU, umesitisha ushiriki wa Madagascar katika umoja huo, baada ya kile ulichokitaja kama mapinduzi nchini humo.

https://p.dw.com/p/HGKV
Kiongozi mpya wa Madagascar, Andry Rajoelina.Picha: picture alliance/dpa


Na kama hii haikutosha, Jumuiya ya maendeleo inayojumuisha mataifa ya kusini mwa mwa Africa, SADC, imesema pia inapangakuweka vikwazo dhidi ya Madagascar. Si kimya pia katika nchi za Magharibi. Ujerumani imeshtumu kubadilishwa kwa utawala nchini Madagascar, na kutaka nchi hiyo irejee katika njia ya demokrasia.


'' Ni mapinduzi,'' ndio uamuzi rasmi wa Umoja wa Afrika, AU, kuhusu mabadiliko ya utawala nchini Madagascar. Na mapinduzi hayachangamkiwi, yanashutumiwa. Baraza la usalama na amani la AU, baada ya mkutano wake wa dharura mjini Addis Ababa, likatoa makali yake...kulitimua taifa hili la kisiwa cha Bahari Hindi kushiriki katika Umoja wa Afrika.


'' Baraza la usalama limeamua ....kusitisha mara moja ushiriki wa Madagascar katika shughuli zote za AU kwa sababu mabadiliko ya kisiasa nchini humo yalikuwa mapinduzi ya kiraia.''

Alisema Bruno Nongoma, balozi wa Burkina Faso, baada ya kuongoza mkutano wa saa mbili wa baraza hilo mjini Addis Ababa, Ethiopia.


AU, pia imegusia iwapo Madagascar haitarea katika siasa zinazoambatana na katiba, basi Jumuiya hiyo haitokuwa na budi, ila kuuwekea utawala wa Rajoelina vikwazo. Na hata kabla ya wino kukauka kufuatia hatua ya AU, SADC ikafuata nyayo. Jumuiya hii ya maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika imemuagiza raia wa Afrika kusini Kglame Motlanthe kuitisha mkutano wa dharura wa SADC kuamua ni vikwazo vipi Madagascar itawekewa.Madagascar ni mwanachama wa SADC.


Kutoka ngazi za kimataifa Ujerumani imeongoza kulaani mabadiliko ya uongozi Madagascar.....Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni alinukuliwa akisema, mabadiliko haya ya uongozi yaliletwa na maandamano, na hii sio njia ya kidemokraisa kubadili serikali. Pia alishtumu hatua ya utawala wa Rajoelina kuvunjilia mbali bunge na kubadilishwa kwa katiba, ili imruhusu awe rais, akisema ni ishara ya muelekeo mbaya, na kwamba lazima Madagascar irejee katika mkondo wa demokrasia.

Katiba ya nchi hiyo ilikuwa imeweka kikwazo cha umri wa mtu anayefaa kuwa rais. Miaka 40. Rajoelina ana umri wa miaka 34.


Mjini Antanarivo, watawala wepya hawakukosa jibu. Kaimu waziri mkuu, Monja Roindefo, alipuuzilia mbali madai kuwa Rajoelina aliingia madarakani kupitia mapinduzi.


'' Nadhani watu wengi hawafahamu nini hasa kilichotendeka Madagascar, lakini tuko tayari kuelezea kwa ufasaha...'' Roindefu aliwajibu wakosoaji wa utawala huu mpya.


Rajoelina, meya wa zamani na wakati mmoja mcheza muziki au ukipenda DJ, aliingia madarakani wiki hii, baada ya miezi miwili ya msukosuko wa kisiasa kati yake na aliyekuwa rais Marc Ravalomanana. Zaidi ya watu 100 waliuawa katika mgogoro huo wa miezi miwili, huku uchumi wa madagascar ukididimia.


Ravalomanana aliyekuwa akihudumu muhula wake wa pili baada ya kuchaguliwa tena kwa miaka mitano, mwaka wa 2006, alisalimu amri pale jeshi lilipoasi na kuondoka mamlakani kwa kukabidhi uongozi jeshi. Jeshi nalo likampa dhamana Andy Rajoelina, ambaye ameahidi yake itakuwa serikali ya mpito, kisha ataitisha uchaguzi katika miaka miwili ijaayo.


Mwandishi:Munira Muhammad/ AFP

Mhariri: Miraji Othman