1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU Kuwaekea vikwazo wanaochochea ghasia Sudan Kusini

Mjahida4 Januari 2014

Umoja wa Afrika umesema utaweka vikwazo kwa wanaochochea ghasia Sudan Kusini, ambako wiki mbili ya mapigano zimesababisha mauaji ya maelfu ya watu.

https://p.dw.com/p/1AjOv
Mmoja ya mwanajeshi wa Sudan Kusini
Mmoja ya mwanajeshi wa Sudan KusiniPicha: Reuters

Baraza la amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetoa taarifa na kusema kwamba iltachukua hatua madhubuti, ikiwemo kuwaekea vikwazo wale wote wanaochochea mapigano ya kikabila nchini humo.

Katika mkutano wa Umoja huo uliofanyika jana mjini Banjul, Gambia wameelezea masikitiko yao kwa taifa hilo jipya na changa kuingia katika mgogoro ambao unahofiwa kushika makali zaidi na kuingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Mapigano Sudan Kusini yalianza Desemba 15 wakati rais wa nchi hiyo Salva Kirr alipomshutumu makamu wa rais wa zamani Riek Machar, kwa kujaribu kupanga mapinduzi dhidi ya serikali yake.

Wanajeshi wa Sudan Kusini wakishika doria katika baadhi ya miji
Wanajeshi wa Sudan Kusini wakishika doria katika baadhi ya mijiPicha: picture-alliance/dpa

Hali hiyo ilichochoea mapigano kati ya Kabila la Dinka anakotokea Rais Salva Kirr na kabila la Nuer la Riek Machar.

Aidha viongozi wa shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la mashariki na pembe ya Afrika IGAD wametaka Salva Kirr na Machar kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana siku ya Jumanne.

Hata hivyo hakuna matumaini yoyote ya wawili hao kukutana leo. Umoja wa Afrika sasa umesema utafanya kazi pamoja na IGAD katika kuwaekea vikwazo wanaochochea ghasia

Makabiliano makali kati ya jeshi na waasi

Huku hayo yakiarifiwa jeshi la Suda Kusini limesema limepambana na waasi walio na nia ya kuudhibiti mji wa Bor. Akizungumza na shirika la habari la AFP msemaji wa jeshi hilo Philip Aguer amesema bado wanasubiri taarifa zaidi juu ya mapigano hayo.

Wiki iliopita jeshi lilifanikiwa kuudhibiti mji huo lakini katika siku za hivi karibuni waasi wamekuwa mbioni kutaka kuuteka tena mji wa Bor ulioko katika jimbo la Jonglei.

waathirika wa mapigano ndani ya kambi ya UNAMIS
Waathirika wa mapigano ndani ya kambi ya UNAMISPicha: Reuters

hali hiyo imesababisha maelfu ya watu kuuhama mji huo kwa hofu ya kuzidi kwa machafuko. Wanamgambo waliotiifu kwa Machar wanaojulikana kama jeshi leupe wanasemekana kujihami kwa bunduki, panga na hata mabomu.

Wanamgambo hao wanajulikana kama Jeshi hilo jeupe , kwa sababu ya kujipaka rangi nyeupe usoni ili kujinusuru na wadudu na pia kama ishara ya kuingia vitani.

Kwa sasa Rais Salva Kirr ameondoa uwezekano wa kugawana madaraka na waasi ili kukomesha umwagikaji damu unaoendelea. Akizungumza na Shirika la utangazaji la Uingereza BBC, Kirr amesema hata hatua ya kuingiliwa kijeshi haitomaliza mgogoro uliopo.

Kirr amesema mtu anayetaka madaraka kamwe hapaswi kuunda makundi ya waasi huku akitoa mfano wake kwamba hakuingoza Sudan Kusini kutokana na mapinduzi bali ni kutokana na chaguo la wananchi wa nchi hiyo.

Riek Machar na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Riek Machar na rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Reuters

Kirr amesema Machar angelisubiri uchaguzi wa mwaka 2015 ili nayeye ateuliwe kihalali.

Rais huyo wa Sudan Kusini amesema wamekuwa wakipigana kwa muda mrefu na kitu kilicho na umuhimu kwa sasa hivi ni kutafuta suluhu ya mgogoro huo ili raia wa Sudan warejee makwao na kuishi kwa amani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed-Abdulrahman