1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN:Assange aachiwe huru

Admin.WagnerD5 Februari 2016

Uamuzi huo wa leo (05.02.2016) unatoa matumaini kwamba Assange huenda akawa huru baada ya kukaa katika ubalozi wa Ecuador mjini London kwa karibu miaka minne.

https://p.dw.com/p/1HqEi
Julian Assange London Botschaft Ecuador
Picha: picture-alliance/dpa/Kerimokten

Jopo la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwamba muasisi wa mtandao wa WikiLeaks, Julian Asaaange, amekuwa akizuia kinyume na sheria na Uingereza na Sweden. Jopo hilo lilitoa taarifa yake ya kurasa 18 mapema Ijumaa na limetaka Assange aachiwe huru na alipwe fidia kwa muda wake wote aliozuiwa tangu Desemba 2010.

Msemaji wa mtandao wa WikiLeaks, Kristinn Hrafnsson, alisema, "Tunatarajia serikali ya Uingereza na serikali ya Sweden kuchukua hatua zinazofaa; kufuta waranti wa kukamatwa dhidi ya Assange na viongozi wa Uingereza wamrejeshee paspoti yake na kumuachia huru kwa kuwa ndilo jambo pekee la busara linaoweza kufikiriwa."

Waendesha mashtaka wa Sweden wanataka kumhoji Assange kuhusiana na madai ya ubakaji wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya nchini humo mwaka 2010, wakati mtandao wa WikiLeaks ulipofichua nyaraka za siri na kuibua gumzo kubwa kote ulimwenguni. Mara kwa mara Assange ameyakanusha madai hayo lakini amekataa kurejea Sweden kukutana na waendesha mashitaka na hatimaye akatafuta hifadhi katika ubalozi wa Ecuador jijini London, ambako mekuwa akiishi tangu Juni 2012.

Katika hatua ambayo ni pigo kwa mfumo wa sheria wa Sweden, jopo la Umoja wa Mataifa liligundua kwamba Assange hakushtakiwa rasmi nchini Sweden, mbali na kuwekwa chini ya uchunguzi wa awali. Mwenyekiti wa jopo hilo Seong-Phil Hong alisema jopo hilo limeamua kwamba aina mbalimbali za kunyimwa uhuru dhidi ya Assange ni kumzuia kinyume na sheria na anastahili haki ya kulipwa fidia.

Kristinn Hrafnsson Wikileaks Sprecher London
Kristinn Hrafnsson, Msemaji wa WikiLeaksPicha: Andrew Cowie/AFP/GettyImages

Carey Shenkman, mmoja wa mawakili wa Assange kutoka Marekani alisema wamefurahishwa na uamuzi wa jopo la Umoja wa Mataifa. "Huu ni ushindi mkubwa kwetu baada ya uchunguzi huru na Umoja wa Mataifa uliofanyika kwa kipindi cha miezi 16. Uingereza na Sweden zilikuwa na muda wa kutosha kuwasilisha ushahidi na ushahidi huo ukazingatiwa na jopo hili na uamuzi ni kuwa mteja wetu alizuia kinyume na sheria."

Shenkman aidha alisema mawakili wote wa Assange waliridhika na taarifa hizo za kusisimua ambazo zilithibitishwa na wizara ya mambo ya kigeni ya Sweden.

Uamuzi wapingwa vikali

Sweden ilisema haikubaliani kabisa na uamuzi wa jopo la Umoja wa Mataifa na uamuzi huo hauna athari yoyote rasmi kisheria kwa uchunguzi unaofanywa dhidi ya Assange kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo. Katika barua iliyoliandikia jopo hilo, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema serikali haikubaliani na tathmini iliyotolewa na idadi kubwa ya wajumbe wa jopo hilo, ikiongeza kwamba chombo hicho hakina haki ya kuingilia katika kesi inayoendeshwa na mamlaka ya umma ya Sweden.

Thomas Olsson, wakili raia wa Sweden anayemuwakilisha Assange, ameitaka Swden izingatie maamuzi yaliyobainishwa katika ripoti ya jopo la Umoja wa Mataifa.

Uingereza nayo ilisema itaupinga rasmi uamuzi huo na kwamba Assange atatiwa mbaroni iwapo atatoka nje ya ubalozi wa Ecuador. Msemaji wa serikali ya Uingereza amesema anachokifanya Assange ni kuzuia kwa hiari kukamatwa kwa kubakia ndani ya ubalozi huo, Amesema madai ya ubakaji na waranti wa kukamatwa kwake ungalipo, kwa hiyo Uingereza ina jukumu kisheria kumrejesha nchini Sweden.

Mawakili wa Assange wanatarajiwa kutoa tamko kuhusu uamuzi wa jopo la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/rtre/ape

Mhariri:Iddi Sessanga