1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu wa Uganda atunukiwa nishani ya amani

1 Oktoba 2012

Juhudi za kuwasaidia maelfu ya watoto waliotekwa kaskazini mwa Uganda na kugeuzwa wanajeshi zimempatia Askofu Mkuu John Baptist Odama tuzo ya amani kutoka shirika la misaada ya kibinaadamu duniani, World Vision.

https://p.dw.com/p/16Hwq
Kiongozi wa LRA, Joseph Kony.
Kiongozi wa LRA, Joseph Kony.Picha: AP

Shati yake inamfanya aonekane kama mtu mwenye ajira. Alama iliyo kwenye mfuko wa mbele wa shati hiyo, inaonesha kuwa Kenneth Ovet ni mwajiriwa wa kampuni ya utengezaji mashine za kupozea joto.

Lakini kijana huyu wa miaka 28 aliinunua shati hiyo mitumbani tu. Bado mwanajeshi huyo wa zamani hajaweza kujifunza biashara na kujenga maisha yake mwenyewe. Maisha aliyoyapitia utotoni, bado hayajaweza kumuacha hadi sasa.

“Nilipotekwa nyara, hicho kilikuwa ni kitu kibaya kabisa kunitokezea. Nilikuwa naogopa sana.” Anasema Kenneth.

Kenneth alikuwa na miaka 11 tu wakati huo. Ni mmoja kati ya maelfu ya watoto walioathirika kutokana na uasi wa kundi la National Resistance Army (LRA) kaskazini mwa Uganda. Kenneth alilazimika kujifunza kupigana na kuua. Ni miaka miwili tu iliyopita ndipo Kenneth alipofanikiwa kuwatoroka waasi, lakini akapigwa risasi wakati akikimbia. Hata hivi leo, akitembea anaburuta mguu wake.

Kenneth akutana na Askofu Odama

Kijana huyo alipata msaada kwa Askofu Mkuu John Baptist Odama, ambaye anawahudumia wale ambao waliwahi kuwa wanajeshi utotoni mwao. Amekuwa pia akijaribu kuwa mpatanishi kati ya waasi wa LRA na serikali ya Uganda.

Kamanda wa LRA, Jenerali Caesar Achellam.
Kamanda wa LRA, Jenerali Caesar Achellam.Picha: Reuters

Mambo yote mawili yamemsababishia kupokea vitisho vya kuuawa mara kadhaa, lakini kamwe hajawahi kutishika. Kutokana na juhudi zake hizo, hivi karibuni alitunukiwa nishani ya amani na shirika la misaada ya kiutu duniani, World Vision.

“Ninapigania amani, sio tu kwa eneo hili bali pia kwa Uganda nzima na kwa bara letu.” Anasema Askofu Mkuu Odama.

John Baptist Odama ni mshauri kwa maana zote. Huzungumza na wanajeshi hao wa zamani kuhusuiana na maisha yao na hasa kile ambacho wanaweza kumuhadithia. Wavulana na wasichana hao ni watu ambao kwa miaka mingi walikuwa wamejifunza kwamba vurugu ndio njia pekee ya kufanikisha jambo lolote lile. Askofu huyo sasa anawahubiria amani.

Matumaini mapya

Askofu huyo ameanzisha kampeni ya kuwaleta pamoja viongozi wa kidini kutoka dini na madhehebu zote. Wakatoliki, Orthodox na Waislamu wanafanya kazi pamoja kuitulizanisha hali kaskazini mwa Uganda.

Mapambano ya Jeshi la Uganda dhidi ya waasi wa LRA.
Mapambano ya Jeshi la Uganda dhidi ya waasi wa LRA.Picha: Ugandan Army

Kazi kubwa iliyo moyoni mwake ni kuwafanya wanajeshi watoto kurudi tena kwenye maisha ya kawaida. Amejenga kituo cha kuwahudumia. Kenneth amefundishwa namna ya kutumia vifaa. Skuli anajifunza kuwa seremala.

Pia amepata mawasiliano tena na mkewe, ambaye alikutana naye kwenye uasi na ambaye amezaa naye mtoto mmoja. Kidogo kidogo kijana huyu wa miaka 28 anaanza kupata uhai mpya.

“Nitajifufua mwenyewe ili niweze kumuhudumia mwanangu, naye aweze kwenda skuli.” Anasema Kenneth.

Kenneth anataka apate kazi haraka iwezekanavyo, na shati yake iandikwe jina halisi la kazi hiyo.

Mwandishi: Antje Diekhans/Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba