1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askari wa NATO wauawa Afghanistan

27 Agosti 2012

Wimbi la mauwaji limeikumba Afghanistan baada ya Askari wa jeshi la nchi hiyo kuwauwa wanajeshi wawili wa vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya na kufikisha idadi ya mashambulizi dhidi ya vikosi hivyo kufikia 12 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/15x9U
Picha: picture-alliance/Ton Koene

Mauwaji hayo ya wanajeshi wa Nato yanafanya idadi ya vifo vya askari wa vikosi hivyo kufikia 42 katika kipindi cha mwaka huu pamoja na kufikisha asilimia 13 ya vifo vyote vya walinda amani wa vikosi hivyo kwa mwaka 2012. Navyo vikosi vya Nato vilijibu mashambulizi hayo na kumuuwa askari huyo. Pamoja na tukio hilo, Raia 17 pia wameuawa kusini mwa nchi hiyo.

Jumuiya ya Nato imekuwa ikipambana kuzuia mashambulizi dhidi ya vikosi vyake yanayofanywa na wanajeshi wa Afghanistan ambao wanashirikiana na vikosi hivyo kulinda amani. Mara kadhaa wanajeshi wa Afghanistan wamekuwa wakiwageuzia kibao washirkika wao na kuwafyatulia risasi.

Bendera za nchi wanachama wa NATO
Bendera za nchi wanachama wa NATOPicha: picture-alliance/ZB

Ingawa kundi la wanamgambo wa Taliban limekuwa likitangaza kuhusika na mashambulizi hayo, lakini Nato inahusisha matukio hayo na tofauti za utamaduni, msongo wa mawazo na uadui baina ya wanajeshi wa Afghanistan na vikosi vya kulinda amani vya jumuiya hiyo.

Mauwaji ya raia 17 na askari 10

Tofauti na Mauwaji ya wanajeshi wa vikosi vya Jumuiya ya Kujihami ya Nato, ISAF, kwenye jimbo la Laghman hii leo, aliyefanya mauwaji ya raia hao 17 kwa kuwachinja bado hajajulikana.

Raia hao wakiwemo wanawake wawili waliuawa kwenye eneo la kusini mwa nchi hiyo katika mji ambao ni maskani ya washambuliaji wa kundi la Taliban. Msemaji wa Jimbo la Helmand ambako ndiko yalikotokea mauwaji hayo amesema kuwa bado wanachunguza chanzo cha mauwaji hayo ingawa kundi la Taliban limetangaza kuhusika.

Kundi la wanamgambo la Taliban
Kundi la wanamgambo la TalibanPicha: dapd

Miili ya watu hao ilikutwa kwenye nyumba moja kiometa 75 kaskazini mwa mji wa Lashkar Gah. Watu hao walikuwa kwenye sherehe za harusi ambazo kundi la Taliban linazipinga kwa kuwa zinawakutanisha pamoja wanawake na wanaume ambao si ndugu.

Wanamgambo wa Taliban wamekuwa wakifanya mauwaji dhidi ya raia kwenye eneo hilo wakiwatuhumu kuwa wanawachunguza ili wakatoe taarifa kwa vikosi vya NATO. Hii ni kutokana na operesheni za hivi karibuni zilizofanywa na vikosi hivyo

Alfajiri ya leo (27.82012) wanamgambo hao walivamia kituo cha ukaguzi na kuwauwa askari 10 wa Afghanistan ambalo linashukiwa kufanywa kwa ushirikiano na baadhi ya wanajeshi wa ndani katika jeshi la Afghanistan. Askari wengine wanne wamejeruhiwa kwenye mashambulio hayo na ambapo sita wengine wamepotea na hawajulikani walipo.

Jeshi la Afghanistan
Jeshi la AfghanistanPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa kutoka vyombo vya serikali zimethibitisha kuwa mashambulizi yanayofanywa na wanamgambo wa kindi la Taliban yanasaidiwa na askari ndani ya jeshi la nchi hiyo. Timu ya wachunguzi imeshatumwa kwenye eneo hilo kuchunguza chanzo cha mauwaji.

Mwandishi: Stumai George/AFPE

Mhariri:Josephat Charo