1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ashton kukutana tena na Yanukovych

Admin.WagnerD5 Februari 2014

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton anatarajiwa kukutana na rais wa Ukraine Viktor Yanukovych wakati upinzani ukimtuhumu rais huyo kwa kujikokota kuhusiana na mapendekezo yao.

https://p.dw.com/p/1B2w4
Rais Yanukovych na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton.
Rais Yanukovych na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton.Picha: picture-alliance/dpa

Katika jitihada mpya za kujaribu kukomesha mkwamo wa karibu miezi miwili kati ya serikali ya upinzani, bunge lilitarajiwa kujadili marekebisho ya katiba ili kupunguza mamlaka ya rais. Na katika tahfifu muhimu kwa vuguvugu la upinzani, rais Yanukovych pia anatafakari kuitisha uchaguzi wa mapema kwa mujibu wa duru za bunge la nchi hiyo.

Waandamanaji wa upinzani mjini Kiev.
Waandamanaji wa upinzani mjini Kiev.Picha: Yuriy Dyachyshyn/AFP/Getty Images

Lakini upinzani unamtuhumu kiongozi huyo wa Ukraine, ambaye anakabiliwa na uchaguzi mwaka ujao wa 2015, kwa kutafuta ushindi badala ya kukomesha machafuko ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa na kuyageuza baadhi ya maeneo ya mji mkuu Kiev kuwa uwanja wa vita.

'Kiongozi asiewajibika'

Baada ya kukutana na Yanukovych kwa duru nyingine ya mazungumzo, bondia wa Ukraine aliegeuka kuwa mwanasiasa Vitali Klitschko alisema rais huyo alimuambia kuwa mageuzi ya kikatiba yanaweza kuchukuwa hadi miezi sita. Klitschko alisema msimamo huo wa Yanukovych unaonyesha kiongozi asiewajibika.

Ashton alipata chakula na viongozi wa upinzani baada ya kuwasili mjini Kiev jana Jumanne, na Klitschko alisema kuwa mwakilishi huyo wa juu wa Umoja wa Ulaya aliwahakikishia kuwa umoja huo uko tayari kutuma ujumbe wa wapatanishi wa ngazi ya juu kwa ajili ya majadiliano na serikali.

Wakati huo huo, Ikulu ya Urusi Kremlin imesema marais Vladmir Putin na Yanukovych wataujadili mgogoro wa Ukraine kandoni mwa sherehe za ufunguzi wa michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mjini Sochi siku ya Ijumaa.

Msemaji wa rais Putin Dmitry Peskov, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa rais Yanukovych atahudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo, na kuthibitisha kuwa wawili hao watakutana na kuzungumzia uhusiano baina ya mataifa yao.

Kiongozi wa upinzani wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akiwa na Catherine Ashton.
Kiongozi wa upinzani wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk akiwa na Catherine Ashton.Picha: picture-alliance/AP

Mapema wiki hii waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Leonid Kozhara alisema rais Yanukovych anapanga kusafiri mjini Sochi kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo.

Wafuasi ya Yanukovych nao wacharuka

Wakati huo huo, wafuasi wa rais Yanukovych wameweka kambi mkabala na walipoweka wapinzani katika uwanja wa Maidan mjini Kiev, wakipaza sauti za kuzuwia kile wanachokiita mapinduzi. Wafuasi hao wa Yanukovych waliokuwa wanapeperusha benedera za chama tawala, wanasema rais huyo ametoa tahifu za kutosha kwa wapinzani na sasa ni wakati kwa wao pia kukutana naye nusu njia.

Mratibu wa kambi hiyo ya wafuasi wa Yanukovych Andriy Kucher mwenye umri wa miaka 27, alisema hawataki kuigeuza Ukraine kuwa kama Syria au Yugoslavia. Kambi hiyo inajulikana kama "Anti-Maida" au kambi dhidi ya Maidan, lakini waandaji hupendelea jina chanya zaidi la Uwanja wa muungano.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Saum Yusuf