1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arsene Wenger apewa mkataba mpya

30 Mei 2017

Kocha wa klabu ya ligi kuu ya England Arsenal, Arsene Wenger amemwambia mmiliki wa klabu hiyo Stan Kroenke kwamba atakubali mkataba mpya wa miaka miwili aliopendekezewa na klabu hiyo, haya ni kulingana na ripoti Jumanne.

https://p.dw.com/p/2dqmx
Arsene Wenger, Coach von Arsenal London
Arsene WengerPicha: AP

Wenger alikutana na Kroenke aliye na kiasi kikubwa cha hisa katika klabu hiyo pamoja na afisa mkuu mtendaji Ivan Gazidis Jumatatu ili kuzungumzia mustakabali wake kabla kandarasi yake haijakamilika mwezi Juni. Wenger mwenye umri wa miaka 67 ameshutumiwa pakubwa msimu huu, huku mashabik wa the gunners wakitaka abwage manyanga baada ya timu yao kushindwa kufuzu katika ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza katika miaka 20.

Tetesi kwamba Arsenal walikuwa wanatafakari kumuandika kazi mkurugenzi wa masuala la soka ili afanye kazi pamoja na Wenger, ni jambo lililozua madai kwmaba Mfaransa huyo alikuwa anafikiria kuufikisha kikomo uhusiano wake wa miaka 21 na Arsenal.

Tangazo rasmi litatolewa Jumatano

Ingawa baada ya kuiongoza Arsenal kunyakua ubingwa wa FA mikononi mwa Chelsea Jumamosi kwa kuwalaza 2-1 uwanjani Wembley mbele ya Kroenke, Wenger alidokeza anataka kusalia kuwa kocha wa Arsenal.

Tangazo rasmi la mkataba mpya aliopewa Wenger unatarajiwa kutolewa Jumatano. "Klabu inapanga kutoa tangazo rasmi Jumatano mchana," alisema msemaji wa klabu hiyo aliyekataa kuthibitisha ripoti za uamuzi wa Wenger.

Italien Neapel v Real Madrid - UEFA Champions League Robert Lewandowski
Arsenal wameshindwa kufuzu katika Champions League msimu ujaoPicha: picture alliance/empics/J. Walton

Wenger ameshinda mataji 3 ya ligi kuu ya England na ameweka rekodi kwa Arsenal kushinda mataji 7 ya FA chini ya uongozi wake, na atahudhuria mkutano wa bodi ya Arsenal Jumanne ambapo kandarasi hiyo inatarajiwa kupigwa muhuri.

Licha ya kuwa Gazidis bado anataka kuwepo na mkurugenzi wa soka hapo Arsenal, Wenger ameambiwa kwamba atasalia kuwa mwenye usemi katika masuala ya kuchagua kikosi kitakachoshiriki mechi na hata uhamisho wa wachezaji.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE

Mhariri: Bruce Amani