1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arkady Babchenko – mtu aliyerejea kutoka kwa wafu

Bruce Amani
31 Mei 2018

Mkosoaji wa serikali ya Urusi Arkady Babchenko ni mtu aliyerejea kutoka kwa wafu. Hivyo ndivyo ilivyoonekana mjini Kiev wakati maafisa waliandamana naye kuzungumza kuhusu "uchunguzi wa mauaji".

https://p.dw.com/p/2yh6g
Ukraine Journalist Arkadi Babtschenko PK in Kiew | mit Lutsenko & Grizak
Picha: Reuters/V. Ogirenko

Mara akajitokeza tena. Mtu ambaye tayari alikuwa ametolewa salamu za rambirambi kutoka kila sehemu na ambaye jina lake liliongezwa kwenye orodha ya kumbukumbu ya wanahabari mjini Moscow saa chache kabla. Arkady Babchenko alirejea kutoka kwa wafu akiandamana na mkuu wa ujasusi wa Ukraine na mwendesha mashitaka mkuu. Mwanahabari huyo alikuwa ametangazwa kuuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake mjini Kiev.

Babchenko mwenye umri wa miaka 41 alivishukuru vikosi vya usalama vya Ukraine kwa kuyaokoa maisha yake kabla ya kumuomba radhi mkewe kwa kumuweka katika hali ngumu kama hiyo. "Nnavyojua ni kuwa operesheni hii ilipangwa kwa zaidi ya miezi miwili, lakini nilifahamishwa mwezi mmoja uliopita. Katika mwezi huu niliona jinsi maafisa walivyofanya kazi, kama walivyofukua mambo kama nyati. Tuliwasiliana mara kwa mara, tukatafakari na kukamilisha mipango".

Ukraine Kiew vorgetäuschter Mord an Journalist Arkadi Babtschenko NEU
Tayari watu walikuwa wanaomboleza kifo cha BabchenkoPicha: Reuters/G. Garanich

Maafisa walifafanua kuwa kitendo hicho cha kudanganya kifo cha mwanahabari huyo kilihitajika ili kuwanyamazisha watu wanaoshukiwa kuamuru na kupanga kumuua mkosoaji huyo wa serikali ya Urusi. Lengo lilikuwa ni kukusanya ushahidi Zaidi unaomhusisha mtu anayedaiwa kutakiwa kufanya mauaji hayo na maafisa wa ujasusi wa Urusi.

Mkuu wa idara ya usalama ya Ukraine Vasily Gritsak alidai kuwa maafisa wa ujasusi wa Urusi walimpa mwanamme mmoja wa Ukraine dola 40,000 kufanya mauaji ya mwanahabari huyo wa Urusi anayeishi uhamishoni. Kifo hicho kilipangwa na mwanahabari huyo na polisi ya Ukraine baada ya kupokea vitisho vya kuuawa. Polisi imesema mshukiwa mmoja amekamatwa

Mauaji ya kisiasa ili kuidhoofisha nchi?

Rais Petro Poroshenko alisifu habari hizo kama ishara kuwa Ukraine "imeupita mtihani wa kuwa nchi huru” na akaiita siku hiyo kuwa "siku ya kuzaliwa” kwa taifa hilo.

Lakini mbali ya duru za serikali kulikuwa na hisia za wazi kwenye mtandao wa intanet za kupongeza mkakati huo wa serikali na utayarifu wake wa kuchukua hatua za hatari.

Ukraine Russischer Journalist Babtschenko lebt
Babchenko alikutana na Rais Poroshenko wa UkrainePicha: Reuters/Ukrainian Presidential Press Service/M. Lazarenko

Lakini vipi kuhusu gharama ya uaminifu wa Ukraine kimataifa? Saa chache baada ya kile kilichoripotiwa kuwa muaji ya Babchenko, Waziri Mkuu Volodymyr Groysman aliituhumu Urusi kuwa utawala wa kikaidi na akatoa wito wa muuwaji wake kuadhibiwa.

Inawezakana kuwa Groysman hakufahamu kilichokuwa kinaendelea? Kwa wakati huo, Waziri wa Mambo ya Nje Pavlo Klimkin alikuwa katika Umoja wa Mataifa mjini New York, ambako alizungumza kuhusu sababu za serikali yake kuamini kuwa Urusi haitaepukana na mauaji ya kisiasa ili kuidhoofisha Ukraine.

Mbinu za msingi

Mbunge Wa Ukraine Anton Gerashenko alisisitiza kuwa matokeo ya kitendo hicho yanahalalishwa kabisa mbinu zilizotumika. Lakini nje ya mipaka ya Ukraine hisia zimekuwa za hasira. Mkuu wa shirika la Maripota Wasio na Mipaka, Christophe Deloire, aliyaita matukio hayo kuwa mabaya mno na ya kusikitisha.

Jukumu sasa lipo mikononi mwa wapelelezi wa Ukraine kuthibitisha kuwa matumizi haya mabaya ya Imani ya umma yalistahili. Watahitaji kuonyesha kuwa kutoweka kwa Babchenko kuliwasaidia wapelelezi kuthibitisha kikamilifu uhusiano kati ya anayetuhumiwa kupanga njama hiyo na maafisa wa ujasusi wa Urusi. Ulimwengu unasubiri.

Mwandishi: Nicholas Connoly
Tafsiri: Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga