Annan ataka serikali ya mseto Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.06.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Annan ataka serikali ya mseto Syria

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za Kiarabu katika mzozo wa Syria Koffi Annan amependekeza iundwe serikali ya mseto nchini humo ikujumlisha wajumbe kutoka pande zote zinazohasimiana.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan.

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan.

Annan ametoa pendekezo hilo siku chache kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu Syria mjini Geneva, Uswis Jumamosi wiki hii. Mkutano huo uliyokubaliwa kufanyika baada ya mzozano baina ya Marekani na Urusi kuhusiana na ajenda zake na orodha ya washiriki, utahudhuriwa na viongozi kutoka baadhi ya serikali za kanda hiyo lakini mahasimu wawili, Iran na Saud Arabia hawatahudhuria.

Shinikizo la kuundwa kwa serikali ya mseto linakuja huku idadi ya vifo inazidi kuongezeka kwa kiwango cha kutisha. Siku ya Jumatano peke yake, watu 149 waliripotiwa kuuawa katika kile waangalizi wa haki za binadamu walisema ndiyo wiki ya umuagaji damu uliyopindukia tangu kuanza kwa mgogoro huo zaidi ya mwaka mmoja uliyopita.

Wachochezi kuwekwa kando

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Serikali inayopendekezwa na Annan itawaweka kando wale wote wanaoonekana kupinga kipindi cha mpito au kuhujumu juhudi za kuleta maridhiano. Mataifa yote makubwa zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, na washirika wa rais Assad, Urusi na China, wanaunga mkono mpango huu ambao utajadiliwa katika mkutano huu wa mawaziri wa mambo ya nje ulioitishwa na Annan.

Lugha ya mpango huu inaashiria kwamba rais Bashar Assad anaweza kuwekwa kando lakini pia baadhi ya maafisa kutoka upande wa upinzani hawataruhusiwa kushiriki katika serikali hiyo. Haya ni kwa mujibu wa Mwanadiplomasia moja wa Umoja wa Mataifa ambaye hata hivyo alisisitiza kuwa hakuna tamko linalomuondoa moja kwa moja rais Assad.

Wanadiplomasia wanasema hatua ya Urusi kukubali mpango huu inaweza kuwa ishara kuwa nchi hiyo iko tayari sasa kumtupa mkono Assad, lakini Balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Vitaly Churkin alisema hakuna uhakika kwamba mpango huu wa Annan utakubaliwa mjini Geneva. Alisema chochote anachokianda Annan kitatumika tu kama msingi wa majadiliano kwa mawaziri.

Uturuki, Qatar, Kuwait na Iraq watahudhuria Mkutano huu. Annan na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon walitaka Iran ishiriki mazungumzo hayo kama ilivyotaka Urusi lakini Marekani inapinga vikali ushirkishwaji wake. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton anatarajiwa kukutana na mwenzake wa Urusi Sergio Lavrov siku ya Ijumaa mjini Saint Petersburg kwa mazungumzo yanayotarajiwa kugubikwa na mgogoro wa Syria.

Mawaziri wa mambo ya nje, Sergey Lawrow wa Urusi na William Hague wa Uingereza.

Mawaziri wa mambo ya nje, Sergey Lawrow wa Urusi na William Hague wa Uingereza.

Wapinzani wasema laazima Assad akae pembeni
Lakini Wapinzani wamesema hawatakubaliana na mpango huo wa Koffi Annan isipokuwa tu kama utakuwa na kifungu cha kumtaka rais Bashar Assad kukaa pembeni. Mjumbe wa Baraza la Taifa la Syria Samir Nashar alisema mpango hauko wazi na kuongeza kuwa kama haumtaki Assad kukaa pembeni basi wao wataukataa.

Wakati huo huo, taarifa znasema Uturuki, ambayo ilisema hapo jana kuwa haina mpango wa kuingia vitani na Syria, imeanza kupeleka vikosi vyake mpakani mwake na Syria katika kile inachosema ni kuchukua tahadhari baada ya Syria kutungua ndege yake Ijumaa iliyopita.

Afisa mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake alithibitisha kuwepo kwa vikosi vya Uturuki katika mkoa wa mpakani wa Hatay na kuongeza kuwa magari ya kivita na makombora ya kutungulia ndege vilikuwa vimewekwa katika maeneo kadhaa katika mkoa huo wa Hatay.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\RTRE\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com