1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Anders Breivik jela miaka 21

Admin.WagnerD24 Agosti 2012

Mtuhumiwa wa mauwaji ya watu 77 nchini Norway Anders Behrings Breivik amehukumiwa kifungo cha miaka 21 jela.

https://p.dw.com/p/15vzX
Picha: Reuters

Majaji watano waliokuwa wanachanguza kama ana matatizo ya akili wamesema akili zake ni timamu na kumhukumu kifungo. Hukumu hiyo imetolewa baada ya wiki 10 za kusikilizwakesi. Breivik alionekana akitabasamu wakati wote ambao jaji kiongozi katika kesi hiyo Wenche Elizabeth Arntsen akisoma hukumu dhidi yake.

Breivik aliwauwa kwa bomu watu wanane mjini Oslo na baadae kuwauwa vijana wengine 69 kwa kuwafyatulia risasi vijana wa chama cha Labour kwenye kambi waliyokuweko karibu na kisiwa cha Utoya Julai 22 mwaka jana.

Wajumbe, jopo la kesi ya Breivik
Wajumbe, jopo la kesi ya BreivikPicha: Reuters

Kisheria Norway haina adhabu ya kifo wala kifungo cha maisha na kiwango cha juu kabisa cha adhabu kwa Breivik ni miaka 21. Hata hivyo wafungwa kama Breivik kama wakionekana kuwa wataendelea kuwa kitisho kwa jamii muda wa kukaa gerezani unaweza kuongezeka.

Amekiri kufanya mauwaji

Breivik mwenye umri wa miaka 33 amekiri kufanya mashambulizi hayo huku akijiona kama shujaa kwa taifa lake ambaye anapambana na uvamizi wa kiislamu barani ulaya na dhidi ya wale wote wanaounga mkono mchanganyiko wa tamaduni.

Anders Breivik akiwa mahakamani mjini Oslo
Anders Breivik akiwa mahakamani mjini OsloPicha: Reuters

Katika hukumu hiyo mahakama iliangalia kigezo kikubwa ambacho ni kama mtu huyo ni mzima wa akili na kama anaweza kuchukuliwa hatua kwa makosa aliyoyafanya. Kwa kutumia ripoti ya jopo la wataalamu wa masuala ya akili waliochaguliwa na mahakama kumchunguza Breivik ambayo ilionyesha ni mzima wa afya, mahakama iliamuru atumikie makosa yake gerezani.

La kushangaza ni kuwa adhabu hiyo ya kifungo gerezani ndiyo ambayo Breivik, familia nyingi za waathirika na umma wa Norway ukiitaka. Breiviki mwenyewe alitaka akutwe mzima wa akili ili siasa zake za kupinga Uislamu zisionekane kuwa zinatokana na maradhi ya akili.

Wasiwasi wa akili za Breivik

Mwendesha mashitaka Svein Holden alitaka mtuhumiwa huyo kuangaliwa kama mgonjwa wa akili na ahukumiwe kwenda jela ya watu wenye matatizo hayo akisema kuwa itakuwa mbaya kumuhukumu kifungo cha kwaida mtu mwenye matatizo ya akili kuliko kumhukumu mtu asiye na matatizo ya akili kwenda jela ya watu wenye matatizo hayo. Breivik aliwahi kusema kuwa hatakata rufaa dhidi ya hukumu atakayopewa.

Anders Behring Breivik
Anders Behring BreivikPicha: Reuters

Akiwa gerezani wakati wa kesi yake, Breivik alipokea barua 100 zenye ujumbe wa kumuunga mkono kwa kitendo chake hicho ambazo zilitumwa na watu kutoka nchi mbalimbali barani Ulaya, wenye siasa kali za mrengho wa kulia na chuki dhidi ya wageni.

Mauwaji aliyoyafanya Breivik yaliitikisa Norway ambayo kwa kiasi kikubwa inafuata siasa za Kiliberali na kuzusha mjadala wa kitaifa kuhusu wafuasi wa mrengo wa kulia, uhuru wa kujieleza na masuala ya uhamiaji.

Mwandishi: Stumai George/AFP/DPAE/Reuters

Mhariri:Moahammed Abdul-Rahman