1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC kumjadili Zuma

Sekione Kitojo
5 Februari 2018

Chama tawala cha ANC kitafanya mkutano wa dharura leo Jumatatu(05.02.2018)kujadili hali ya baadaye ya rais Jacob Zuma baada ya  kuzungumza usiku wa jana na kiongozi anayeandamwa na kashfa kushindwa kumshawishi kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/2s8HK
Südafrika Pretoria - Südafrikanischer Präsident Jaboc Zuma
Picha: Reuters/S. Sibeko

Jacob Zuma , ambaye  yuko  madarakani  tangu mwaka  2009 , amekabiliwa  na  mbinyo unaozidi  kuongezeka  akitakiwa  ajiuzulu tangu  pale  nafasi  yake  ya  uongozi  wa  chama  cha  ANC kuchukuliwa  mwezi  Disemba  na  Cyril Ramaphosa, ambaye  ni makamu  wake  wa  rais. Chama  cha  ANC  kiliitisha  kamati  ya taifa  ya  utendaji  kukutana  katika  makao  makuu  ya  chama katika  jengo  la  Luthuli  mjini  Johannesburg kwa  majadiliano.

Südafrika Emmerson Mnangagwa, Simbabwe & Jacob Zuma in Pretoria
Mwenyekiti wa ANC Cyril Ramaphosa (Kushoto) na rais wa Afrika kusini Jacob Zuma(kulia)Picha: Reuters

Ili  chama  hicho  kiweze  kumlazimisha  Zuma  kujiuzulu  kama rais wa  nchi , kamati  hiyo  italazimika  kuitisha  mkutano  wa  kamati kuu  ya  taifa, ikiwa  ni  chombo  chake  kikuu  cha  maamuzi, kupiga kura  kumuondoa  Zuma.

Maafisa  sita  wa  ngazi  ya  juu  wa  chama  cha  ANC  walikutana na  Zuma  usiku  wa   jana  Jumapili  katika  makao yake  rasmi mjini Pretoria lakini  hakuna  tangazo  lililotolewa  kuhusiana  na  kikao hicho.

Kiongozi  wa  upinzani  Julius Malema, mwanachama  wa  zamani wa  ANC, amesema  Zuma amekataa kujiuzulu  katika  mkutano  huo Jumapili  usiku.

"Amekataa  kujiuzulu  na  aliwaambia  wachukue  uamuzi  kumuondoa iwapo wanataka  kufanya  hivyo  kwa sababu  hajafanya  chochote kibaya  kwa  nchi  hiyo'', Malema aliandika  katika  ukurasa  wa Twitter.

Julius Malema
Julius Malema mwanachama wa zamani wa ANCPicha: dapd/AP Photo/Themba Hadebe

Waungaji  mkono  kuandamana

Katika  ishara  ya  Zuma  kung'ang'ania madarakani, kundi la waungaji  wake  mkono linalojulikana  kama  Waafrika  kwanza  nchi kwanza , wamesema  wataandamana  hadi  katika  jengo  la  Luthuli leo  Jumatatu. Kwa  upande  mwingine , kundi  linalomuunga  mkono Ramaphosa   la  chama  tawala  cha  ANC limesema  litalilinda  jengo hilo, na  kuzusha  uwezekano  wa  mapambano  kati  ya  kambi tofauti za  ANC.

Südafrika Cyril Ramaphosa, neuer Präsident ANC
Wanachama wa ANC wakifurahia kuchaguliwa kwa Cyril RamaphosaPicha: Reuters/R. Ward

Zuma ametengwa  na  washirika  wake  muhimu tangu  Ramaphosa alipokuwa  kiongozi  wa  chama  pekee  kuiongoza  Afrika  kusini tangu  kumalizika  kwa  utawala  wa  Wazungu  wachache  mwaka 1994. Ramaphosa, mwenye  umri  wa  miaka  65  yuko  katika nafasi  nzuri  ya  kuwa  rais  ajaye  na  amekuwa  akiweka ushawishi  wake ili  Zuma  aondolewe madarakani.

Zuma  hajasema  iwapo  atajiuzulu kwa  hiari  kabla  ya  muda  wake wa  muhula  wa  pili  kama  rais  kumalizika  mwaka  ujao. Vyama vya  upinzani  na  baadhi  ya  wanachama wa  ANC wanataka aondoke  kabla ya  hotuba  ya  hali  ya  taifa  hilo  katika  bunge, hotuba  iliyopangwa  kutolewa  hapo Alhamis.

Südafrika ANC Parteitag Ramaphosa
Kiongozi wa ANC Cyril RamaphosaPicha: Getty Images/AFP/G. Khan

Zuma ameponea  mara  kadhaa  kuondolewa  madarakani  katika kura  za  kutokuwa  na  imani  nae  wakati  wa  utawala  wake kutokana  na  kura  za  utiifu  kwake  za  wabunge  wa  chama  cha ANC, lakini  uungaji  mkono  wa  uongozi  wake  unapungua. licha  ya kuwa  Zuma  anaendelea  kuungwa  mkono  na  baadhi  ya  makundi ndani  ya  ANC, hashikilii  tena  wadhifa  wa  juu.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Daniel Gakuba