1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yadai kufanyika uhalifu wa kivita Mosul

Bruce Amani
11 Julai 2017

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International likizishutumu pande zote katika vita ya kuukomboa mji wa Mosul nchini Iraq kwa kukiuka sheria ya kibinadamu.

https://p.dw.com/p/2gJIv
Irak Kampf um Mossul gegen den IS
Picha: Getty Images/A. Al-Rubaye

Shambulizi moja la angani lilipiga kitongoji kimoja cha Mji Mkongwe katika jiji la Mosul, hali iliyosababisha wingu kubwa la moshi. Makombora ya IS yalianguka karibu na maeneo ya jeshi la Iraq na milio ya risasi ilirindima katika upande wa magharibi wa mji huo wa kale. Matukio hayo yanadhihirisha hatari ambayo bado inatokana na wanamgambo hao baada ya wanajeshi wa Iraq kutangaza kuchukua udhibiti kamili wa Mosul, mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq, ikiwa ni miaka mitatu baada ya kukamatwa na wanamgambo hao wa itikadi kali waliokuwa na lengo la kutangaza Dola la kiislamu ulimwenguni.

Amnesty International imesema leo kuwa jeshi la Iraq na jeshi la muungano linaloongozwa na Marekani katika vita dhidi ya IS mjini Mosul yalikiuka kila mara sheria ya kimataifa ya kibinaadamu na huenda yalifanya uhalifu wa kivita.

Irak, Der irakische Premierminister Haider al-Abadi hält eine irakische Flagge, als er den Sieg über den islamischen Staat in Mosul verkündet
Iraq ilitangaza ushindi kamili dhidi ya IS mjini MosulPicha: Reuters

Kundi hilo la haki za binaadamu pia limesema IS lilivunja sheria ya kimataifa kwa kuwatumia maelfu ya raia kama ngao za binaadamu na kutowaruhusu kuondoka mjini humo. Pia wanamgambo hao waliwauwa mamia au hata maelfu ya raia waliojaribu kukimbia.

Hapo jana, Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alizuru Mosul kwa siku ya pili mfululizo na akatangaza rasmi ushindi, ikiwa ni karibu miezi kumi baada ya mchanganyiko wa wapiganaji wa Kikurdi, wanajeshi wa Iraq na wanamgambo wa Kishia kuanzisha operesheni ya kulifurusha kundi la IS kutoka mji huo "Tuna kazi nyingine ambayo ni ya kurejesha utulivu, ujenzi mpya na kuliangamiza kundi la IS na hii inahitji juhudi za usalama na ujasusi na umoja wetu. Kama tu tulivyoungana katika vita vyetu dhidi ya IS tunahitaji kuungana tena ili kurejesha utulivu katika eneo hili na kuwarejesha nyumbani waliopoteza makazi na kujenga maeneo yote ambayo yalikombolewa"

Sehemu kubwa ya Mosul hasa mji wa kale wenye idadi kubwa ya watu, imeharibiwa wakati jeshi la serikali ya Iraq likishiriki mapambano makali ya mtaa mmoja hadi mwingine likisaidiwa na mashambulizi ya angani ya jeshi la muungano.

Irak Kampf um Mossul
Maelfu ya raia walikimbia makazi yao kutokana na vitaPicha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Amnesty imesema wanajeshi wanaoiunga mkono serikali ya Iraq walitumia silaha zisizofaa katika mapigano ya maeneo ya mijini, ikiwa ni pamoja na makombora

Kuijenga upya Mosul na kuwasaidia raia bado ni changamoto kubwa. Mashirika ya misaada yanaonya kuwa mzozo wa kibinaadamu nchini Iraq utaendelea huku ufadhili ukipungua. Umoja wa Mataifa unasema mzozo wa kiutu nchini Iraq hautamazilika hivi karibuni. Umesema karibu watu 920,000 wameachwa bila makazi na maelfu hawataweza kurudi makwao kwa sababu ya uharibifu mkubwa uliofanywa.

Ushindi wa kijeshi dhidi ya IS pia unazusha uwezekano wa kutokea tena uhasama wa makundi kadhaa ya kisiasa na migogoro ambayo iliwekwa kando wakati wa vita hivyo.

IS ilitwaa mji wa Mosul mnamo Juni 2014 na kutangaza Dola la kiislamu wakati ikijitanua hadi Iraq na Syria hali iliyolazimu operesheni ya kijeshi wa Marekani ambao kisha baadaye ilitanuliwa kutokea Iraq hadi Syria.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel