1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Jeshi la Nigeria liliwaua raia 347

John Juma22 Aprili 2016

Amnesty International linasema uchunguzi wao ulibaini wanajeshi walienda kinyume na sheria walipoamua kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji hao ambao hawakuwa na silaha. Jeshi halijawasilisha ushahidi kujiondolea lawama.

https://p.dw.com/p/1Ial4
Wanajeshi wa Nigeria
Wanajeshi wa NigeriaPicha: picture-alliance/dpa/H. Ikechukwu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelilaumu jeshi la Nigeria kwa kufyatua risasi kiholela na kuua waislamu 350 wa Madhehebu ya Shia na kuwazika katika makaburi ya pamoja kisha kuharibu ushahidi wa uhalifu huo.

Kadhalika shirika hilo limepuuzilia mbali madai ya jeshi la Nigeria kuwa waandamanaji wa vuguvugu hilo la Kiislamu- Islamic Movement of Nigeria (IMN) lilitaka kumwua mkuu wa majeshi kabla ya makabiliano Disemba mwaka jana.

Mara kwa mara jeshi la Nigeria limeshukiwa kukiuka haki za raia katika vita vyake dhidi ya wanamgambo wa madhehebu ya Sunni wa Boko Haram. hata hivyo jeshi hilo limekuwa likisema wanajeshi wake hufanya kazi yao kwa njia sawa.

Kumekuwepo na hofu kuwa matendo ya jeshi hilo dhidi ya kundi la Shia eneo la Zaria yanaweza kuzua mapigano mengine kama ya Boko Haram ambayo yameshasababisha vifo vya watu 20,000 tangu mwaka 2009.

Machafuko yaliyodumu kwa siku mbili tangu Disemba 12, yalianza pale wafuasi wa vuguvugu la IMN wanaomuunga mkono kiongozi wa kidini Ibrahim Zakzaky walizuia msafara wa mkuu w amajeshi kupita katika eneo la sherehe iliyokuwa ikihudhuriwa na kiongozi huyo wa kidini anayeunga mkono sera za Iran.

Amnesty International linasema uchunguzi wao ulibaini wanajeshi walienda kinyume na sheria walipoamua kufyatua risasi dhidi ya waandamanaji hao ambao hawakuwa na silaha.

Jeshi imeshindwa kutoa ushahidi kujitetea

Kwenye ripoti hiyo ninanukuu "Haijitokezi wazi ni kwa nini jeshi lilifanya operesheni hiyo ya kijeshi katika hali ambayo ilikuwa tulivu na salama kisheria. "Ripoti imeongeza kuwa jeshi liliwateketeza watu wakiwa hai, wakachoma nyumba na kuitupa miili katika makaburi ya pamoja. Kisha kuosha alama za damu, kuokota maganda ya risasi zilizotumiwa.

Eneo la Zaria nchini Nigeria
Eneo la Zaria nchini NigeriaPicha: picture-alliance/dpa/Stringer

Wiki iliyopita afisa mmoja wa serikali alisema watu 347 miongoni mwao watoto na wanawake walizikwa katika kaburi la pamoja chini ya usimamizi wa jeshi, shughuli iliyoidhinishwa na mahakama.

Licha ya ahadi ya rais Muhammadu Buhari kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa kumaliza visa kama hivyo.

Zakzaky ambaye alipoteza jicho lake na kupooza sehemu ya mwili wakati wa ghasia hizo, amekuwa kizuizini bila kuwasiliana hata na mawakili, hadi alipoachiliwa hivi majuzi. Awali amewahi kufungwa jela kwa kutaka mapinduzi kama ya Iran ili kuunda taifa la kiislamu kaskazini mwa Nigeria.

Mwandishi: John Juma/ AFPE

Mhariri:Yusuf Saumu