1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International: Syria inafanya uhalifu dhidi ya binaadamu

Admin.WagnerD14 Juni 2012

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limeituhumu Syria kwa kufanya uhalifu dhidi ya binaadamu kwa lengo la kuuzima upinzani.

https://p.dw.com/p/15EQ4
Free Syrian Army members raise their weapons and a revolutionary flag during a training session on the outskirts of Idlib, Syria, Thursday, June 7, 2012. (Foto:AP/dapd)
Freie syrische Armee Syrien Bürgerkrieg Training Rebellen IdlibPicha: AP

Katika ripoti yake yenye kurasa 70 iliyopewa jina la "Maandamano yaliyokabiliwa na ukandamizaji mkali wa serikali" Amnesty International inasema ina ushahidi wa namna serikali inavyowauwa watu wanaowaunga mkono waasi kwa kutumia mabomu ya kutegwa kwenye magari pamoja na mashambulizi ya kinyama.

Waathirika zaidi kwenye mauwaji hayo ni watoto ambao wanatolewa majumbani mwao kisha kupigwa risasi na askari wa vikosi vya serikali na baadae baadhi ya miili yao kuchomwa moto.

Shirika hilo limewahoji raia kadhaa kwenye vijiji 23 nchini Syria na kuthibitisha kuwa vikosi vya serikali na wanamgambo wanaoiunga mkono ndio wanaohusika na mauwaji ya kinyama yanayofanyika nchini humo.

Wasyria wanajiuliza kwa nini wameachwa?

Afisa aliyewasilisha ripoti hiyo Donatella Rovera anasema kuwa Wasyria wengi wanajiuliza kwa nini hali inazidi kuwa mbaya huku mataifa yakiangalia

"Raia wengi wamechanganyikiwa. Wanaeleza kile kinachowapata wakiwa na matumaini kuwa mataifa yakisikia basi hatua zitachukuliwa. Swali moja la msingi ambalo kila niliyeongea naye alikuwa ananiuliza ni kwanini ulimwengu umetulia na haufanyi chochote wakati sisi tunachinjwa?" alisema Rovera

Ripoti hiyo imetolewa siku moja baada ya serikali kusema kuwa haiko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe bali inawaondoa magaidi hasa kwenye eneo la al-Haffe linalokaliwa na madhehebu ya sunni kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Eneo hilo ni ngome ya Jeshi Huru la Waasi wa Syria, FSA, ambapo watu 80 wameuawa kuanzia jana hadi leo.

Wanaharakati wa Amnesty International wakiwa kwenye maandamano
Wanaharakati wa Amnesty International wakiwa kwenye maandamanoPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa tayari waangalizi wa kimataifa wameingia kwenye eneo hilo la al-Haffe baada ya kuzuiwa kwa siku mbili na vikosi vya usalama serikali. Siku ya Jumatatu Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumiya ya Nchi za Kiarabu-Arab League Kofi Annan alisema ana wasiwasi huenda raia kwenye eneo hilo wamezingirwa na mauwaji yanaendelea.

China yaendelea kumtetea Assad asivamiwe kijeshi

Wakati Amnesty International likitoa ripoti hiyo kuhusu mauwaji China nayo imeeendelea na msimamo wake wa kupinga hatua za kijeshi kuchukuliwa dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China Liu Weimin alisema kuwa kwa hali ilivyo sasa nchini Syria, kitu cha muhimu ni kuziunganisha pande zinazotofautiana ili ziutii mpango wa amani wa Annan na si matumizi ya nguvu.

Hii leo watu 11 wameuawa kutokana na mapigano kwenye miji wa Idlib na Damascus yalioambatana na miripuko ya mabomu. Taarifa zinasema kuwa vikosi vya serikali vimelizunguka eneo la Tareek al-Sad hii na muda wowote mashambulizi yatafanywa.

Moja ya miripuko nchini Syria
Moja ya miripuko nchini SyriaPicha: dapd

Tangu vuguvugu la kuupinga utawala wa Assad lianze mienzi 15 iliyopita, kiasi ya watu 14,000 wamekwishauawa nchini Syria huku Umoja wa Mtaifa ukisem,a nchi hiyo sasa imo kwenye vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP

Mhariri: Saumu Yusuf