1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amani imepungua duniani

Saumu Mwasimba
6 Juni 2018

Utafiti unaonesha kwamba amani imepungua katika nchi nyingi duniani,hasa Mashariki ya Kati na nchi za Afrika Kaskazini kufuatia migogoro inayoendelea na kusababisha wakimbizi.

https://p.dw.com/p/2z0rU
Demonstration in Nantes Frankreich
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Dovarganes

Amani duniani imepungua ikilinganishwa na hali ilivyokuwa muongo mmoja uliopita. Sababu kubwa ya kushuhudiwa hali hiyo ni migogoro inayoendelea Mashariki ya kati na barani Afrika ambayo imeugharimu uchumi wa dunia dola trillioni kadhaa.

Mkuu wa taasisi ya uchumi na amani (IEP) yenye makao makuu yake nchini Australia, Steve Kilelea anasema kwamba amani duniani imekuwa ikipungua taratibu kwa kipindi cha muongo mmoja na kinachochangia hali hiyo ni migogoro Mashariki ya kati, na Afrika ya kaskazini ambayo athari zake zimevuka mipaka na kuingia kwenye maeneo mengine ya dunia.

Ulaya kuna amani zaidi

Ulaya imekabiliwa na mgogoro mkubwa wa wakimbizi tangu mwaka 2015 kufuatia vita nchini Libya na Syria. Zaidi ya watu millioni 1 kutoka Afrika na Mashariki ya kati pamoja na kutokea Afghanistan wamejaribu kufika barani Ulaya kupitia Uturuki au kupitia njia ya bahari.

Infografik Global Peace Index 2018 EN
Ramani inayoonesha viwango vya amani vya nchi

Taasisi hiyo ikitumia data za taasisi za utafiti na vyuo vikuu kutoa uchambuzi wake inakadiria kwamba vurugu zilizotokea katika mwaka 2017 katika maeneo mbali mbali ya dunia, zimeugharimu uchumi dola trilioni 14.8 ikiwa ni sawa na mtu mmoja kupoteza kiasi  ya dola 2000. Endapo nchi ambazo hazina usalama kama vile Syria, Sudan Kusini, na Iraq zingekuwa na utulivu katika hali ilivyo katika nchi zenye amani  kama vile Iceland na New Zealand ina maana kila mmoja uchumi wake ungeongezeka kwa dola 2000.

Kilelea anasema huo ndio utafiti pekee uliofanywa ambao unapima athari za vita katika uchumi wa dunia. Ulaya imeorodheshwa kama eneo lenye utulivu zaidi duniani wakati Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini yakitajwa kuwa maeneo yenye usalama mdogo. Nchi tano zimetajwa kuwa na amani  zaidi ni Newzeland, Iceland, Austria, Ureno na Danemark.

Mizozo inazigharimu nchi

Ujerumani bado hali haijabadilika ikiwa katika nafasi ya 17, lakini pia kati ya nchi 36 za Ulaya nchi 23 zimetajwa kwamba hali imekuwa mbaya katika kipindi cha mwaka uliopita. Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Mei ulisema kwamba mgogoro wa kibinadamu nchini Syria umeongezeka mwaka huu kuliko ilivyowahi kushuhudiwa wakati mwingine wowote wa vita nchini humo ambavyo vimedumu miaka 7.

Ruanda Kiziba Flüchtlingslager
Wakimbizi wa Congo wakiwasili RwandaPicha: Reuters/J. Bizimana

Katika nchi jirani ya Iraq kundi linalojiita dola la Kiislamu IS, linasababisha kitisho kikubwa katika mipaka ya Syria licha ya kwamba nchi hiyo ilitangaza ushindi wa mwisho mnamo mwezi Desemba dhidi ya wapiganaji hao wa itikadi kali waliokuwa wakiithibiti thuluthi moja ya Iraq. Nchi 104 zimepunguza asilimia ya pato jumla la nchi zao ya fedha zinazotumika katika bajeti ya kijeshi wakati nchi 115 zimepunguza idadi ya wanajeshi.

Eneo la Afrika Kusini mwa jangwa la sahara ndilo lenye idadi kubwa ya watu walioachwa bila makaazi ndani ya nchi zao kutokana na vurugu na migogoro katika kipindi cha mwaka uliopita.Kwa mujibu wa ripoti ya kituo kinachofuatilia watu walioachwa bila makaazi katika nchi zao kuna nusu ya watu millioni 11.8 walioachwa bila makaazi duniani wako katika eneo hilo la Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.

Mwandishi: Von Hein Matthias/Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo