1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyeshambulia Düsseldorf ana matatizo ya kiakili

10 Machi 2017

Polisi nchini Ujerumani wamemkamata mtu mmoja anayeaminika kuwa na matatizo ya kiakili aliyewashambulia na kuwajeruhi watu saba katika kituo cha treni cha Düsseldorf usiku wa Alhamis.

https://p.dw.com/p/2YwiM
Deutschland Axtangriff am Düsseldorfer Hauptbahnhof
Polisi nje ya kituo cha treni cha Düsseldorf baada ya shambuliziPicha: Getty Images/A. Scheuber

Kulingana na watu walioshuhudia tukio hilo, mtu huyo mwenye umri wa miaka 36 kutoka iliokuwa Yugoslavia, alishuka kutoka kwenye treni na kuanza kuwashambulia watu hovyo na kuacha damu ikiwa imetapakaa kila mahali.

Makomando wa polisi waliojihami wakisaidiwa na helikopta za polisi walikimbilia sehemu hiyo ya tukio na kumkamata mtu huyo aliyekuwa anaruka kutoka darajani ili asikamatwe.

Msemaji wa polisi mapema Ijumaa aliwaambia waandishi wa habari wameondoa uwezekano wa lengo la kigaidi katika shambulizi hilo na kwamba mtu huyo alifanya shambulizi hilo pekeyake. Wachunguzi awali walisema kwamba mtu huyo hakuwa sawa kiakili na ni suala hilo lililompelekea kufanya shambulizi hilo. 

Kituo kilifungwa ili uchunguzi kufanywa

"Mwendo wa saa tatu kasoro dakika kumi usiku, tulikuwa na hali ya kutoeleweka lakini watu saba walijeruhiwa, miongoni mwao wanawake wawili. Tumemkamata mtu aliyewashambulia na tumelizuia shoka alilotumia. Abiria wote walitolewa kwenye treni na kupelekwa nje," alisema msemaji wa polisi mjini Düsseldorf Markus Niescery.

Verletzte bei Axt-Attacke im Düsseldorfer Hauptbahnhof
Polisi waliojihami walifika kwa harakaPicha: picture-alliance/dpa/D. Young

Kituo cha Düsseldorf kilifungwa na huduma katika kituo hicho kusitishwa kwa muda huku treni zikiamrishwa kutumia njia mbadala kabla kituo hicho kufunguliwa tena baada ya saa sita usiku.

Kulifanyika uchunguzi wa kina katika kituo hicho na hata katika baadhi ya treni jambo lililowalazimu abiria kusalia ndani kwa muda wote huo.

Mashambulizi kama haya yamewahi kutokea Ujerumani awali

Meya wa mji huo Thomas Geisel, alieleza kusikitishwa kwake na shambulizi hilo na akatuma rambirambi kwa kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter, "fikra zetu ziko kwa wale wote waliojeruhiwa baada ya tukio hilo baya katika kituo kikuu cha treni cha Düsseldorf. Shukran kwa huduma zote za dharura."

Hii si mara ya kwanza kwa shambulizi kama hili kutokea nchini Ujerumani, kwani mwezi Julai mwaka jana, kijana aliye na umri wa miaka 17 aliyekuwa anatafuta hifadhi aliwashambulia kwa kisu na shoka abiria katika treni karibu na mji wa Wuerzburg, na kuwajeruhi watu watano.

Kulingana na idara za usalama nchini Ujerumani, takriban watu 10,000 wamepokea mafunzo ya itikadi kali za Kiislamu na 1,600 kati yao, wana uhusiano na makundi ya kigaidi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga