1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yatangaza vita dhidi ya uharamia

Bruce Amani
16 Oktoba 2016

Viongozi wa Afrika wamepongeza kutiwa saini muafaka wa kihistoria wa kuimarisha ulinzi wa pwani za bara hilo katika jaribio la kuzuia uharamia na biashara ya magendo

https://p.dw.com/p/2RGz8
Somalia Piraterie
Picha: picture-alliance/AP

Rais wa Jamhuri ya Congo, Denis Sassou Nguesso amesema makubaliano hayo ya Umoja wa Afrika ni ya "kihistoria", wakati mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta akisema yalionyesha uwezo wa Afrika kuufanikisha mkakati mpana. Maafisa wanasema mataifa 43 yameidhinisha makubaliano hayo katika mkutano wa kilele ulioandaliwa katika mji mkuu wa Togo, Lome.

Chini ya mkataba huo, taasisi kadhaa zitaundwa ili kupambana na uhalifu wa baharini ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa watu na silaha kimagendo. Aidha mataifa ya Afrika yatabadilishana taarifa, mapungufu ambayo yamewanufaisha maharamia katika siku za nyuma, kwa kuendesha shughuli zao baharini bila matatizo. Kati ya mataifa 54 wanachama wa Umoja wa Afrika – AU, 38 yana mwambao wa pwani.

Wanajeshi wa Ufaransa wakiwakamata maharamia wa Kisomali katika Ghuba ya Aden
Wanajeshi wa Ufaransa wakiwakamata maharamia wa Kisomali katika Ghuba ya AdenPicha: Verteidigungsministerium/AFP/Getty Images

Mazungumzo hayo yaliwaleta pamoja viongozi wa nchi 18 – idadi isiyo ya kawaida kwa mkutano wa AU wa aina hii, kuashiria umuhimu ambao serikali zimeweka kwenye umuhimu wa kuuzia uharamia na uhalifu mwingine wa baharini. Wakati akiufungua mkutano huo, Rais wa Chad Idriss Deby, mwenyekiti wa sasa wa AU, alisema kuwa asilimia 90 ya bidhaa zinazoingia na kutoka nje zinazosafirishwa baharini, hali inayofanya usalama wa safari za majini kuwa muhimu katika mustakabali wa kiuchumi barani humo. Deby alisema muafaka huo "utawezesha kukuza biashara na utumiaji wa uwezo mkubwa wa sekta ya baharini, pamoja na kukuza utajiri na kazi katika sekta nyingine za kibiashara”. Pia utakuwa ni "hatua mpya muhimu katika juhudi za kuhifadhi mazingira ya baharini”, aliongeza.

Lakini Timothy Walker, mtafiti wa usalama wa baharini katika Taasisi ya Masomo ya Usalama – ISS alisema muafaka huo utaziwezesha nchi kutotoa taarifa kwa kila mmoja kama zitahisi hilo kuwa ni katika maslahi ya usalama wa kitaifa.

Manowari ya Urusi katika Bahari ya Hindi
Manowari ya Urusi katika Bahari ya HindiPicha: AFP/Getty Images/S. D`Souza

Uharamia, biashara ya magendo na uhalifu mwingine wa baharini umeigharimu sekta ya bahari barani Afrika mamia ya mabilioni ya dola katika miongo ya karibuni, kwa mujibu wa AU. Uvuvi haramu wa kiwango kikubwa pia unachangia katika ongezeko la uharamia kwa sababu unapunguza hifadhi za samaki, na kupunguza shughuli halali za kiuchumi katika jamii za pwani.

Katika Afrika Magharibi pekee, AU inakadiria kuwa uvuvi haramu unasababisha hasara ya dola milioni 285 kila mwaka. Uharamia umepungua ulimwenguni tangu 2012 baada ya operesheni za doria za meli za kimataifa kuzinduliwa katika pwani ya Afrika Mashariki kutokana na mashambulizi yaliyofanywa sana sana na maharamia wa Kisomali.

Lakini sasa uharamia umehamia katika Ghuba ya Guinea ambako wanamgambo wanaotokana na kundi la waasi wa Niger Delta wanaendesha shughuli zao. Muafaka huo utahitaji kuridhiwa na karibu nchi 15 kabla ya kuanza kutekelezwa na Barthelemy Blede, mtafiti wa masuala ya baharini katika taasisi ya ISS nchini Cote d'Ivoire anasema itasubiriwa kuona kama kutakuwa na "nia ya kweli” ya kuufanikisha mkataba huo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo