1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yajipanga kuwa na jeshi la dharura

6 Novemba 2013

Viongozi wa Kiafrika wameanza mazungumzo ya kuunda kikosi cha dharura barani humo kwa ajili ya kuingilia migogoro inayozuka kwa sasa, wakati wakisubiri mpango wa pamoja wa bara zima kuwa na kikosi maalum cha jeshi.

https://p.dw.com/p/1ACu3
Wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
Wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).Picha: picture-alliance/dpa

Mkutano wa kilele unaohudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu wa bara hilo - wakiwemo wa Chad, Tanzania na Uganda - mjini Pretoria, Afrika ya Kusini, ni kuiwezesha Afrika kuingilia kati haraka na ikiwa inajitegemea katika changamoto za kiusalama zinazolikabili bara hilo, kwa mujibu wa mwenyeji wa mkutano huo, Rais Jacob Zuma.

"Uamuzi huu umetokana na kutambua kwamba uingiliaji kati kwenye migogoro yetu wenyewe hauwezi kusubiri hadi Kikosi Maalum cha Dharura cha bara zima kiundwe," alisema Zuma.

Hatua za pole pole

Uundwaji wa kikosi hicho maalum cha Umoja wa Afrika umekuwa ukisuwasuwa tangu mapendekezo yake ya kuwa na wanajeshi 32,500 na raia kutoka kanda tano za bara hilo kuanza muongo mzima uliopita.

Wanajeshi nchini Niger.
Wanajeshi nchini Niger.Picha: STR/AFP/Getty Images

"Tunaamini kwamba wakati wa viongozi wa Kiafrika kuweza kuchukua hatua za mpito, za usalama na za kimaamuzi zinapohitajika umefika," alisema Zuma.

Umoja wa Afrika ulikosolewa kwa kutochukuwa hatua za haraka dhidi ya mgogoro wa Mali baada ya jeshi kuchukua madaraka mwezi Machi 2012, na sasa viongozi hao wanasema wanataka kuhakikisha kwamba hawaonekani wasio uwezo au walio nyuma sana katika kuchukua hatua bila ya msaada wa mataifa ya nje.

Dhamira mpya

Wanajeshi katika mitaa ya Niger.
Wanajeshi katika mitaa ya Niger.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

"Afrika inaweza na ina uwezo na njia za kuchukua hatua. Tunachohitaji ni kujipanga wenyewe tu," alisema Rais Zuma kwenye mkutano huo.

Inategemewa kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu "kutakuwa na mfumo unaoweza kuhuisha dhamira yetu ya kuwa na umiliki na uongozi wetu wenyewe katika kukabiliana na changamoto za kiusalama kwenye bara letu tukufu."

Mkutano huo unahudhuriwa na nchi ambazo zimesema ziko tayari kuchangia kwenye kikosi hicho, Haikufahamika mara moja ni nchi ngapi kwa sasa ambazo zimeahidi kutuma wanajeshi wake kuunda kikosi hicho, ambacho kitaitwa "African Capacity for Immediate Response to Crises (ACIRC)."

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Josephat Charo