1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Afrika si tena bara linaloomba msaada tu"

Maja Dreyer10 Desemba 2007

Mkutano kati ya nchi za Kiafrika na za Umoja wa Ulaya ulimalizika Lisbon jana, kwa hakika, ni mada iliyopewa kipaumbele na wahariri wa magazeti ya humu nchini.

https://p.dw.com/p/CZow
Bendera za nchi zilizoshiriki kwenye mkutano wa LisbonPicha: AP

Kwanza ni wa gazeti la “Die Welt” ambalo linatathmini hotuba ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani. Gazeti limeandika:

“Badala ya njia ya kidiplomasia ya kuzungumzia ukosoaji kwenye mikutano ya ndani, Angela Merkel huko Lisbon alitaja wazi juu ya sera za Zimbabwe zinazoharibu uchumi na kukiuka haki za binadamu. Bila shaka, si Mugabe wala dikteta mwingine anayependa kusikia hivyo. Kinachosikitisha hapa ni kwamba viongozi wote wengine wa Afrika walimuunga mkono Mugabe. Lini basi viongozi hao watasita kulalamika tu juu ya mambo ya ukoloni na kukubali sera zao zipimwe kulingana na viwango vya kimataifa?”


Hivyo ndivyo anavyouliza mhariri wa gazeti la “Die Welt”. Mwenzake wa “Stuttgarter Zeitung” anakumbusha kwamba:

“Afrika si tena bara linaloomba msaada tu. Hapana. Siku hizi, China ina maslahi yake ya kiuchumi huko Afrika, na Marekani inataka kuasisi kituo kikuu cha jeshi kwa bara hilo. Ulaya iko nyumba katika mashindano haya juu ya Afrika. Kwa sasa, nchi za Ulaya zina mikakati miwili. Upande mmoja kuna Kansela Merkel wa Ujerumani ambaye anataka kuwa mshirika anayeaminika kwa kuzungumzia wazi ukosoaji wake kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu. Upande mwingine kuna rais Sarkozy wa Ufaransa ambaye anawaahidi viongozi wa nchi za Afrika Kaskazini biashara kubwa na kujenga mitambo ya nyuklia. Sera zitakazoshinda hatimaye bila shaka ni zile za Sarkozy.”


Tunaendelea na gazeti la “Handelsblatt” la mjini Düsseldorf ambalo limeandika hivi:


“Ugomvi huu kati ya viongozi wa Afrika na wale wa Ulaya si kitu kinachoshtusha. Kwani haifai kuwaahidi Waafrika ushirikiano wa ana kwa ana, lakini kuingilia kati katika mambo yao ya ndani. Hii haimaanishi kwamba Mugabe asikosolewe, lakini ukosoaji huu ungepaswa kwenda pamoja na kujikosoa wenyewe. Pia kwenye sekta ya biashara inabidi kuanza upya kabisa. Kuyalazimisha mataifa ya Kiafrika kukubali mikataba hiyo ya EPA kati ya Umoja wa Ulaya na bara hilo lilikuwa wazo baya.”


Kwa mujibu wa mhariri wa “Rhein-Zeitung” wa kutoka Koblenz, mkutano huu wa Lisbon umeonyesha wazi kitu kimoja, nacho ni kwamba:

“Shakashaka dhidi ya dola za ukoloni za zamani ni kubwa. Inabidi nchi za Ulaya zitoe ushahidi kwamba ziko tayari kabisa kulisaidia bara la Afrika liendelee kweli. La sivyo, China na wengine watapata nguvu kubwa mno. Masuala muhimu ni kushirikiana katika uhamiaji, utunzaji wa hali ya hewa na upatikanaji wa nishati - yaani maslahi ya kimkakati. Ulaya inaitegemea Afrika. Pindi hilo limefahamika litekelezwe kama sera nzuri kuelekea bara la Arika ambalo linazidi kujivunia hususan katika wakati ambapo mali ghafi zinapungua duniani kote.”