1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika na wadhifa wa Ujerumani kama mwenyekiti wa G-20

Oumilkheir Hamidou
3 Desemba 2016

Kansela Angela Merkel aitaja Afrika kuwa kauli mbiu ya Ujerumani kama mwenyekiti wa G-20,tuhuma za Rwanda dhidi ya Ufaransa na kufungwa kambi za wakimbizi za Dadaab nchini Kenya ni miongoni mwa mada magazetini wiki hii

https://p.dw.com/p/2Tg7j
Deutschland Angela Merkel & Uhuru Kenyatta in Berlin
Picha: Reuters/H. Hanschke

Tuanzie lakini mjini Berlin ambako decemba mosi iliyopita, Ujerumani ilikabidhiwa zamu ya mwenyekiti wa jumuia ya mataifa 20 yanayoongoza kiuchumi. Mali inapelekea watu kuvutiwa,linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine katika ripoti yake yenye kichwa cha maneno "Serikali kuu ya Ujerumani yaligundua bara la Afrika." Sauti zinapazwa kudai uandaliwe mpango wa msaada kama ule uliotolewa na Marekani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia,Marchal Plan. Lakini suala ambalo Frankfurter Allgemeine linajiuliza ni jee misaada ya maendeleo inasaidia kwa kiwango gani?

Kwa vyovyote vile,linaendelea kuandika Frankfurter Allgemeine,kansela Angela Merkel anasema Afrika itakuwa kauli mbiu ya zamu ya Ujerumani kama mwenyekiti wa jumuia ya nchi zinazoongoza kiuchumi duniani,G20. Hata waziri wa fedha,Wolfgang Schäuble ambae  gazeti hilo linasema,kawaida jukumu lake ni kukusanya fedha,anashangiria fikra ya ushirikiano. Misimamo yote hiyo miwili imechochewa na maelfu ya watu wanaosheheni ndani ya mitumbwi wakiyatia hatarini maisha yao katika bahari ya kati kwa lengo la kuingia Ulaya.

Ujerumani yazidisha kiwango cha misaada ya maendeleo kwa Afrika

Kuna wanaoliangalia bara la Afrika kuwa ni bara la matumaini,lakini wanaoyatia hatarini maisha yao wanasema hawaogopi kufa,wanakimbia maisha ya shida,umaskini,matumizi ya nguvu na rushwa katika nchi zao. Ujerumani kama mwenyekiti wa G-20 itafanya nini ili kuwasaidia watu hao na  kuwapatia matumaini mema. Frankfurter Allgemeine linasema Kansela Merkel anashughulika na hali namna ilivyo katika bara jirani tangu muda mrefu na anazungkwea na wataalam wanaomshauri kuhusu njia gani ni borea zaidi kwa bara la Afrika. Gazeti limekumbusha pia kuhusu safari za kansela mwezi Oktoba uliopita nchini Ethiopia,Mali na Niger,na pia ziara zilizofuatia za marais wa Nigeria na Chad mjini Berlin.

Frankfurter Allgemeine linamalizia ripoti yake kwa kukumbusha jinsi Ujerumani ilivyozidisha msaa wa maendeleo kwa Afrika: Pekee katika mhula huu, bajeti ya waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller imeongezeka kwa Euro bilioni mbili.

 Mvutano kati ya Rwanda na Ufaransa kuhusu mchango wa Ufaransa katika mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994

Mada ya pili magazetini inahusu shutuma za Rwanda dhidi ya Ufaransa."Anatafutwa mkosa" ndio kichwa cha maneno cha gazeti la mjini Münich,la Süddeutsche. Gazeti linakumbusha watu zaidi ya laki nane waliuliwa na wahutu mnamo mwaka 1994 nchini Rwanda. Ufaransa wakati ule ilituma silaha katika nchi hiyo iliyokuwa imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na ndio maana hii leo inalaumiwa kuficha makosa yake.

Uhusiano kati ya Ufaransa na Rwanda  tangu zamani ni tete na hivi sasa ndio kabisa baada ya mwendesha mashitaka mkuu wa Rwanda kuanzisha uchunguzi dhidi ya raia 20 wa Ufaransa kwa tuhuma za kuchangia katika mauwaji ya halaiki  kati ya April hadi Julai mwaka 1994. Raia hao 20 wa Ufaransa ,ambao hawakutajwa kwa majina,wametakiwa wajieleze kwanza kabla ya Rwanda kuamua kama washitakiwe au la. Tuhuma za Rwanda zimefuatia uamuzi wa waendesha mashitaka wa Ufaransa walioamua kuchunguza upya sababu za kifo cha rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana,wakidhamiria kumhoji mshirika wa zamani wa rais wa sasa wa Rwanda,anaedai kuwa rais Kagame binafsi anahusika na kudunguliwa ndege aliyokuwa akisafiria Juvenal Habyarimana.

Wasomali waihama shingo upande kambi ya wakimbizi ya Dadaab

Ripoti yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii imeandikwa na gazeti la mjini Berlin die Tageszeitung na kuzungumzia jinsi shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR linavyowashughulikia wakimbizi wa kisomali wanaolazimika kuihama kambi ya Dadaab nchini Kenya. Gazeti linazungumzia kisa cha familia ya Amin Mohammed,mkewe na watoto wao saba. "Buriyani ya huzuni" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalochambua jinsi wakimbizi wanavyolazimika kuweka saini zao kabla ya kupatiwa cheti kinachoonyesha msaada wa chakula na cha pili cha nambari ya simu ya shirika la Mpango wa Chakula wa Umoja wa mataifa nchini Somalia.

Die Tageszeitung linakumbusha kwamba Amin Mohammed ,sawa na wakimbizi wengine ameihama Somalia miaka 25 iliyopita na kukimbilia Kenya vita viliporipuka nchini humo. Kambi ya Dadaab,inayotajikana kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi ulimwenguni,imeamuliwa akufungwa kabisa mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse

Mhariri:Josephat Charo