1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
11 Mei 2018

Juhudi za Ufaransa zenye lengo la kuchangia katika ustawi wa bara la Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba idadi ya kampuni za Ufaransa imeongezeka nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/2xWTN
Boris Becker
Picha: picture-alliance/Mandoga Media

Frankfurter Allgemeine

Mjasiramali kutoka Ufaransa Gregoire Schwebig mwenye umri wa miaka 32 amesema hakuweza kuuona mchakato wa ustawi wa uchumi barani Asia, kwa sababu bado alikuwa mtoto  wakati huo. Lakini sasa anataka kushuhudia kwa macho yake ustawi wa uchumi barani Afrika na ndiyo sababu yeye na mkewe waliamua kufungua biashara nchini Kenya na wako huko tangu mwaka wa 2011. Kwa mujibu wa gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine, Mfaransa huyo, anafanya kazi ya kusanifu  majengo, kuzitafutia kampuni ofisi na kuratibisha shughuli za wafanyabiashara na mahoteli. Schwebig aliliambia gazeti hilo kwamba anaamini bara la Afrika litashuhudia ustawi mkubwa lakini gazeti hilo pia linatilia maanani.

Biashara ya maua maarufu nchini Kenya
Biashara ya maua maarufu nchini KenyaPicha: DW

Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita idadi ya kampuni za Ufaransa nchini Kenya zimeongezeka mara nne na kufikia 80. Ufaransa pia inashika nafasi ya pili kwa kutoa mikopo kwa Kenya katika msingi wa uhusiano baina ya nchi hizi mbili Ufaransa pia inashika nafasi ya nne kwa uwekaji vitega uchumi nchini Kenya.

Die Zeit

Huko huko nchini Kenya gazeti la Die Zeit linazungumzia juu ya suala la ukabila, katika makala yake gazeti hilo linasema ukabila una uzito mkubwa katika siasa, nchini Kenya na linaeleza. Makabila ndiyo yenye uzito mkubwa nchini Kenya na siyo vyama vya kisiasa. Lakini Kenya ni nchi iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo barani Afrika. Ni nchi yenye tabaka la kati kubwa na watu wenye moyo wa ujasirimali. Hata hivyo nchini Kenya usasa bado unaenda sambamba na ukale. Gazeti hilo la Die Zeit limemnukulu mtaalamu wa masuala ya utamaduni nchini Kenya, Kimani Njogu akieleza kuwa ukabila ulipaliliwa na wakoloni.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga

Katika njama zao za kuzuia umoja wa Waafrika wakati huo wakoloni wa Kiingereza waliwatengansisha watu katika msingi wa makabila. Gazeti la Die Zeit linasema kila kabila lilitengewa sehemu yake, na kutokana na sera hiyo mipaka iliwekwa baina ya watu, na hivyo ndivyo msingi wa ukabila ulivyojengwa nchini Kenya. Hata hivyo katika kipindi cha kuelekea kwenye uhuru, ilionekana kana kwamba makabila yalihitajika ili kujiandaa kisiasa na hapo mwanzoni Wakikuyu na Wajaluo walishikana wakati wa kupigania uhuru. Lakini gazeti hilo linakumbusha katika makala yake kwamba njia ya kuelekea kwenye mamlaka ilisababisha mvutano baina ya makabila hayo. Gazeti la Die Zeit limemnukulu mtaalamu Kimani Njogu akisema ukabila ni njama inayotumika kudumisha mamlaka.

die tageszeitung

Katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo gazeti la die tageszeitung linatuarifu kwamba wafungwa kwenye jela moja hawataki kwenda nyumbani hata baada ya kumaliza kutumikia kifungo. Jee ni kwa nini? Gazeti hilo linatueleza kwamba katika jela ya Osio iliyoko karibu na jiji la Kisangani la kaskazini mashariki mwa Kongo ilijengwa na wakoloni wa Kibelgiji mnamo mwaka 1958.

Moja kati ya maeneo ya machimbo ya madini nchini Kongo
Moja kati ya maeneo ya machimbo ya madini nchini KongoPicha: Getty Images

Hata hivyo mkuu wa idara ya sheria katika jimbo la mashariki la Tshopo, Gerard Kombozi alishangazwa alipotambua kwamba wafungwa walikuwa wanakataa kuondoka. Uchunguzi ulibainisha kwamba karibu na jela hiyo wakaazi wameanza kuchimba almasi. Gazeti la die tageszeitung linasema baadhi ya wafungwa na walinzi waliungana na kujenga mji karibu na jela na wafungwa hao na walinzi wanafanya biashara ya madini katika mji huo kwa sababu wana uhuru wa kujisimamia wenyewe.

Bild Zeitung

Makala ya gazeti la Bild inatufahamisha juu ya aliyekuwa mcheza tennis maarufu duniani, Boris Becker wa Ujerumani na ajira yake mpya. Gazeti hilo linatufahamisha zaidi kwamba Jamhuri ya Afrika ya Kati imemwajiri Boris Becker kuwa balozi wake.

Mcheza tennis wa zamani maarufu Boris Becker
Mcheza tennis wa zamani maarufu Boris BeckerPicha: picture alliance/EPA/dpa/Hayoung Jeon

Becker pia anatarajiwa kuwa mwambata wa michezo na utamaduni kwenye Umoja wa Ulaya, na kutokana na uteuzi huo  atakuwa na hadhi ya kidiplomasia. Becker amaeahidi kutumia mitandao yake ya kimataifa pamoja  na mahusiano yake na watu mashuhuri ili kuisaidia Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo