1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo29 Juni 2007

Baadhi ya mada zilizoripotiwa na magazeti ya Ujerumani juma hili: Mkutano wa kimataifa kuhusu mzozo wa Darfur wafanyika mjini Paris Ufaransa. Hali ya kiuchumi nchini Zimbabwe yaendelea kuwa mbaya. Rais wa Nigeria Umaru Yar´Adua ataka kufanya mazungumzo na waasi wa Niger Delta. Na miji mikubwa barani Afrika yakabiliwa na idadi kubwa ya wakaazi.

https://p.dw.com/p/CHSZ

mkutano kuhusu mzozo wa Darfur uliofanyika mjini Paris Ufaransa Jumatatu tarehe 25 mwezi huu, gazeti la Neue Zürcher lilisema Ufaransa iliutumia mkutano huo kudhihirisha uwezo wake kidiplomasia katika kukabiliana na hali ngumu za kibinadamu. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice alihudhuria mkutano huo kuiunga mkono serikali mpya ya Ufaransa ikiongozwa na rais Nicolas Sarkozy.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alihudhuria pia mkutano huo miongoni mwa wajumbe kutoka nchi 20 na mashirika ya kimataifa. Lakini serikali ya Sudan na Umoja wa Afrika haukushiriki kwenye mkutano huo kama walivyofanya wajumbe wa makundi ya waasi wa jimbo la Darfur. Pande hizo zilikataa kushiriki katika mkutano huo kwa sababu hazikushauriwa awali kuhudhuria kikao hicho cha mjini Paris. Rais Nicolas Sarkozy aliitolea mwito serikali ya Sudan na makundi ya waasi yarejee kwenye meza ya mazungumzo ili kuumaliza mgogoro wa Darfur.

Nalo gazeti la Tageszeitung lilisema inatia moyo kuona juhudi kubwa zinazofanywa kutaka kuutanzua mzozo wa Darfur, ingawa bado hakuna dalili za mlango wa kusherehekea kumalizika mzozo huo. Hatua ya Ufaransa kuandaa mkutano kuhusu Darfur inaashiria vipi serikali ya Sarkozy inavyotaka kuishinikiza serikali ya Sudan. Mhariri anasema hatua ya serikali ya Sudan na Umoja wa Afrika kutoshiriki kwenye mkutano huo uliyadhoofisha mazungumzo ya mjini Paris hivyo hakuna mengi yaliyofikiwa.

Mada ya pili inahusu hatua ya rais wa Nigeria Umaru Yar´Adua kutaka kukutana na waasi wa eneo la Niger Delta. Gazeti la Süddeutsche lilisema rais huyo alimuachilia huru kiongozi wa waasi wa Niger Delta, Dokubo Asari, kutoka gerezani, kama ishara ya kutaka kuzungumza na waasi hao. Waasi wa Niger Delta waliitaka serikali ya Nigeria imuachilie kiongozi huyo kabla kuanza mazungumzo. Wanaitaka serikali itumie dola bilioni 40 ya pato la mauzo ya mafuta zitumike kuliendeleza eneo la Niger Delta ambalo wakaazi wake wanaishi katika umaskini uliokithiri, huku gavana wa jimbo hilo akijinufaisha peke yake. Mpaka sasa bado wakaazi wa Niger Delta wanasubiri shule, barabara na umeme.

Mada ya tatu inazungumzia hali mbaya yakiuchumu nchini Zimbabwe huku mfumuko wa bei ukiendela kuongezeka nchini humo. Mhariri wa gazeti la Neue Zürcher aliuliza, je rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anataka kuukwamisha uchumi wa nchi yake? Uchumi wa Zimbabwe umeendelea kuporomoka katika wiki kadhaa zilizopita. Mfumuko wa bei uliripotiwa kufikia kima cha asilimia 4,500 mnamo mwezi Mei mwaka huu, lakini kwa mujibu wa makadirio yaliyotolewa na benki za Afrika Kusini, kima hicho sasa kimefikia asilimia 9,000, huku dola ya Zimbabwe ikiendela kupoteza thamani yake kwa kasi kubwa. Mhariri alimalizia kwa kusema ingawa upinzani nchini Zimbabwe umeshindwa kumuondo rais Mugabe madarakani, kuporomoka kwa uchumi kunaweza kuiangusha serikali yake na hivyo kusababisha mabadiliko ya utawala mjini Harare.

Miji mikubwa imelemewa na idadi kubwa ya waakazi katika nchi zinazoendelea. Hayo yaliripotiwa na gazeti la Süddeutsche. Mhariri alisema watu bilioni moja duniani kote wanaishi kwenye mitaa ya walalahoi katika miji mikubwa. Idadi ya wakaazi kwenye mijini humo inaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa. Kwa mujibu wa ripoti kuhusu idadi ya wakaazi duniani iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, mwaka ujao nusu ya idadi ya wakaazi bilioni 3,3 duniani itakuwa imehamia katika miji. Thuluthi moja kati yao wanaishi katika mitaa ya madongo poromoka.

Gazeti la Süddeutsche lilimnukulu Renate Bähr wa wakfu wa Weltbevölkerung, mjini Berlin, wakati wa kutolewa ripoti hiyo, akisema miji mikubwa barani Afrika imelemewa kabisa na idadi kubwa za wakaazi. Nchini Ethiopia na Uganda kwa mfano asilimia 90 ya idadi ya wakaazi wanaoishi mijini wanaishi kwenye mitaa ya walalahoi.