1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wazuka tena Sudan Kusini

31 Julai 2016

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kurejea tena kwa umwagikaji damu nchini Sudan kusini , na juu ya kuanza kuchongoa tena kwa mlima wa madeni katika nchi za Afrika

https://p.dw.com/p/1JZBR
Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr na Riek Machar aliekuwa Makamu wake ,ambae amemtimua
Rais wa Sudan Kusini Salva Kirr na Riek Machar aliekuwa Makamu wake ,ambae amemtimuaPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Gazeti la "die tageszeitung" linasema damu inamwagika tena katika Sudan Kusini.Linasema sasa ni wazi na rasmi,kwamba hakuna tena amani katika nchi hiyo baada ya Rais Salva Kirr kumtimua makamu wake Riek Machar.

Gazeti la "die tageszeitung" linaeleza kwamba Rais Kirr aliichukua hatua hiyo baada ya majeshi ya Riek Machar kuingia katika mji mkuu, Juba na kupambana na majeshi ya serikali karibu wiki mbili zilizopita. Mamia ya watu waliuawa kutokana na mapigano hayo.

Gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha kwamba Riek Machar aliachishwa kazi kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 2013 kwa kisingizio kwamba alikuwa anafanya njama za kuipindua serikali ya Salva Kirr.

Hatua hiyo ilisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini Machar alirudishwa tena kuwa Makamu wa Rais mnamo mwezi wa Aprili , mwaka huu baada ya kufikiwa mkataba wa amani uliopaswa kuvimaliza vita nchini Sudan Kusini.Lakini gazeti la "die tageszeitung" linasema kutimuliwa kwa Riek Machar maana yake ni kuvunjika rasmi kwa mkataba wa amani nchini Sudan Kusini.

Madeni ya Afrika yaongezeka tena

Gazeti la Süddeutsche Zeitung" wiki hii limelinukulu shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia biashara na mandeleo,UNCTAD likitahadharisha juu ya kuongezka tena kwa madeni ya nchi za Afrika.

Murugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa Mukhisa Kituyi
Murugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa Mukhisa KituyiPicha: picture alliance/AP Photo

Gazeti hilo linasema uchumi wa nchi za Afrika ulikuwa unastawi kwa viwango vya juu, kutokana na bei nzuri za malighafi, zilizuouza kwenye soko la dunia.Lakini tangu bei hizo zianguke, madeni ya nchi za Afrika yalianza kuongezeka tena.

Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha kwamba Mkurugenzi wa shirika la biashara na maendeleo,UNCTAD , Mukhisa Kituyi ameelezea wasi wasi juu ya hatari ya kupanda juu tena kwa mlima wa madeni barani Afrika.

Limemnukulu Bwana Kituyi akieleza kuwa kuchukua mikopo kutoka ndani na nje , kunaweza kusaidia katika kuleta maendeleo ya nchi, lakini inapasa kuwa macho ili madeni yasiongezeke haraka na kuwa makubwa.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema wasi wasi wa mkurugenzi huyo unaweza kueleweka. Linasema ni kweli kwamba nchi za Afrika bado hazijavuka mipaka katika kuchukua mikopo, lakini tangu kuanguka kwa bei za malighafi, na tangu kufumuka kwa mgogoro wa uchumi duniani,madeni ya nchi za Afrika yameongezeka haraka.

Hadi mwishoni mwa mwaka wa 2013 madeni ya nchi hizo kwa pamoja yalifikia Dola Bilioni 443. Gazeti la "Süddetsche" linafahamisha kwamba hadi mwaka wa 2013 madeni ya Kenya na Tanzania yalifikia asilimia 19 ya pato jumla la ndani.

Ujerumani kumkunja samaki angali mbichi

Gazeti la "Berliner " linafahamisha juu ya mpango wa Umoja wa Ulaya na Ujerumani wa kuwazuia wakimbizi wa Afrika,kwenda Ulaya.

Gazeti hilo linasema wakimbizi hao watazuiwa kabla hata ya kufika kwenye bahari ya Mediterania.Linasema Umoja wa Ulaya na Ujerumani zinataka tatizo hilo lipatiwe ufumbuzi ndani ya nchi za Afrika.

Gazeti la "Berliner "limemnukulu Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere akitoa mwito wa kuanzisha utaratibu kama ule unaotumika nchini Uturuki, ambako wakimbizi wanazuiwa kuendelea na safari ya kwenda Ulaya. Gazeti la "Berliner" linafahamisha kwamba nchi mbili zinalengwa katika mpango wa Umoja wa Ulaya na Ujerumani- Libya na Niger.

Gazeti hilo limezikariri takwimu za shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya uhamiaji IOM, zinazofahamisha kwamba wakimbizi wapatao robo Milioni kwa sasa wamelundikana nchini Libya wakisubiri kuondoka.

Kuhusu Niger gazeti linaarifu,kwamba Ujerumani inafanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo ili wawadhibiti wakimbizi wanaojaribu kupitia katika ardhi ya nchi yao .Na kwa ajili hiyo Rais wa Niger Mahamadou Issaofou alialikwa nchini Ujerumani, mwezi juni ambako alifanya mazungumzo na Kansela Angela Merkel.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Yusuf Saumu