1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ntaganda akana mashtaka ya uhalifu

7 Septemba 2015

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya kuanza kusikilizwa kesi ya Bosco Ntaganda anaekabilwa na mashataka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu

https://p.dw.com/p/1GRym
Aliekuwa mbabe wa kivita Bosco Ntanganda mahakamani mjini The Hague
Aliekuwa mbabe wa kivita Bosco Ntanganda mahakamani mjini The HaguePicha: Reuters/M. Kooren

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema Ntaganda amefikishwa kwenye mahakama ya ICC ya mjini the Hague, kujibu mashtaka ya kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu lakini ameyakana mashtaka hayo.


Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaarifu kwamba Bosco Ntaganda pia anakabiliwa na mashtaka ya kuwatumia watoto kama askari, kuwanyanyasa wanawake kingono na kuhusika na mauaji ya wanakijiji zaidi ya 800 ,mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo mnamo mwaka wa 2002.

Gazeti la "Süddeutsche" linakumbusha kwamba,mshtakiwa huyo alikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kurudi nchini ,Rwanda ambako alijisalimisha kwenye ubalozi wa Marekani mnamo mwaka wa 2013. Gazeti hilo linasema kwake yeye Ntaganda, kufikishwa mahakamani mjini The Hague, ni hatari ndogo tu!

Gazeti la "die tageszeitung pia linatilia maanani kwamba Ntaganda amefikishwa mahakamani, mjini The Hague lakini ameyakana mashtaka yote aliyosomewa. Gazeti hilo linafahamisha kwamba kesi ya Ntaganda imepangwa kufanyika kwa miezi kadhaa na watu zaidi ya 70 wataitwa kutoa ushahidi mjini The Hague dhidi ya Ntaganda.

Filamu juu ya Daktari Mukwege yapigwa marufuku

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limeripoti juu ya filamu iliyopigwa marufuku kuonyeshwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Daktari Denis Mukwege aliewatibu wanawake waliobakwa nchini Kongo
Daktari Denis Mukwege aliewatibu wanawake waliobakwa nchini KongoPicha: Reuters/V. Kessler

Filamu hiyo inayoitwa "Mtu aliewarekebisha akina mama" imekuwa inaonyeshwa kwa miezi kadhaa katika sehemu mbalimbali za dunia. Filamu hiyo ni juu ya daktrari Deni Mukwege aliewatibu wanawake waliobakwa mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti la "die tageszeitung" linafahamisha kuwa daktari Mukwege ametunukiwa matuzo mbalimbali ya kimataifa kwa kazi yake nzuri.Na kutokana na kazi hiyo nzuri filamu fupi imetengezwa juu yake. Lakini Jumatano iliyopita ilifafamika kwamba serikali ya Kongo ilikataa kutoa ruhusa ili filamu hiyo ionyeshwe nchini humo.


Gazeti hilo limevikariri vyombo vya habari vya nchini Kongo, vilivyomnukulu Waziri wa habari na msemaji wa serikali akisema kwamba filamu hiyo inawaonyesha watu wanaotoa kauli zinazowakashifu wanajeshi ambazo hazina ushahidi.

Gazeti la "die tageszeitung" limemnukulu msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,Lambert Mende akisema kwamba yale yaliyosemwa katika lugha ya kiswahili na kufasiriwa katika lugha ya kifaransa yalipotoshwa.Wanawake kadhaa wanozungumza katika filamu hiyo wanatoa madai juu ya kubakwa na wanajeshi wa Kongo.

.Gazeti la "Der Tagesspiegel" wiki hii limeandika juu ya kupungua kasi ya ustawi katika uchumi wa China na jinsi nchi za Afrika zinavyoweza kuathirika.

Gazeti hilo linasema uchumi wa nchi za Afrika sasa unapaswa ujiweke sawa kuzihimili athari zinazotokana na kupungua kwa bei za malighafi na kutokana na kupungua kwa vitega uchumi kutoka China. Kupungua bei ya mafuta ulikuwa ujumbe wa kwanza juu ya kupungua kwa kasi ya ustawi wa uchumi wa China.


Gazeti la "Der Tagesspigel" linaeleza kwamba, kuanguka kwa bei ya malighafi kama shaba na chuma na kutokana na kupunguzwa kwa thamani ya sarafu ya China , Yuan ustawi wa uchumi katika nchi za Afrika umefikia mwisho. Gazeti hilo linakumbusha kwamba uchumi wa nchi hizo umekuwa unastawi mtindo mmoja katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaarifu kwamba Angola ndiyo itakayoathirika kwa kiwango kikubwa na mgogoro wa uchumi wa nchini China.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Khelef