1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya26 Aprili 2013

Wiki hii, magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya hatari ya kurejea vita nchini Msumbiji baada ya miaka ishirini ya amani.Na pia yamendika juu ya ustawi wa biashara baina ya Afrika na Ujerumani.

https://p.dw.com/p/18O2V
Mradi wa shule unaofadhiliwa na Madonna,Malawi
Mradi wa shule unaofadhiliwa na Madonna,MalawiPicha: Getty Images/AFP

Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha makala juu ya hatari ya kuvurugika kwa amani nchini Msumbiji baada ya miaka 20 ya utulivu na maendeleo ya kutia moyo nchini humo.

Gazeti la "die tageszeitung" linatupasha habari kwamba kundi la Renamo ambalo lilikuwa linapigana vita vya msituni dhidi ya serikali ya Frelimo nchini Msumbiji limeibuka tena nchini humo.Gazeti la "die tageszeitung" linasema kundi hilo sasa linatishia kuanzisha tena mapigano dhidi ya serikali ya Msumbiji.

Gazeti hilo linaeleza kwamba sababu ya Renamo kutaka kuanzisha tena vita ni kutokuwepo haki katika ugawanaji wa utajiri wa nchi.

Mazungumzo yashindikana:

Gazeti la "die tageszeitung" limearifu kwamba hatua za kwanza za kujaribu kuanzisha mazungumzo baina ya serikali na Renamo zilikanyaga patupu wiki iliyopita.Gazeti la "die tageszeitung" pia limearifu kwamba mashambulio kadhaa yalifanywa na Renamo katika wiki zilizopita na watu watatu waliuawa.

Renamo ilianzisha uasi dhidi ya serikali ya Msumbiji mnamo mwaka 1975 hadi yalipofikiwa mapatano ya kumaliza vita mnamo mwaka wa 1992.

Biashara-Ujerumani na Afrika

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii limechapisha makala juu kustawi kwa biashara baina ya Ujerumani na nchi za Afrika. Katika makala yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemkariri Mwenyekiti wa chama cha biashara baina ya Ujerumani na Afrika Christoph Kannengießer akisema kuwa chama chake kinayaona mapambazuko barani Afrika. Takwimu zinayathibitisha matumaini hayo.Kampuni za Ujerumani zinazofanya biashara barani Afrika zimewaajiri watu karibu laki 2. Mwaka jana Ujerumani iliuza barani Afrika bidhaa thamani ya Euro Bilioni 21,8 na kwa upande wake Ujerumani iliagiza kutoka Afrika bidhaa thamani ya Euro Bilioni 23.9

Mwenyekiti wa chama cha biashara baina ya Afrika na Ujerumani amesema bara la Afrika litakuwa eneo la pili litakaloinukia kiuchumi.

Malawi na Madonna:

Gazeti la "Berliner Zeitung" limeripoti juu ya mvutano kati ya serikali ya Malawi na mwanamuziki maarufu Madonna. Jee kimetokea nini hasa? Gazeti la "Berliner Zeitung" linafahamisha zaidi.

Mwimbaji huyo mashahuri, Madonna alifanya ziara nyingine nchini Malawi hivi karibuni iliyoishia katika patashika kati yake na serikali ya nchi hiyo. Kutokana na nia njema ya kusaidia Madonna alitoa dola laki nne kwa ajili ya ujenzi wa shule. Lakini katika siku ya ufunguzi,mbele ya Madonna mwenyewe, Waziri wa elimu wa Malawi Eunice Kazembe alisema kuwa Madonna alitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kadhaa tu na siyo shule nzima.

Gazeti la "Berliner "limemnukuu Waziri huyo akisema kwamba Madonna hajatimiza ahadi nyingi alizoziweka.Gazeti hilo limearifu kwamba baada ya kuwaasilia watoto wawili kutoka Malawi,yaani kuwachukua na kuwalea kwa hiari, Madonna aliahidi kujenga nchini Malawi chuo cha wasichana thamani ya dola milioni 15 .Lakini ahadi hiyo haijatimizwa linasema gazeti la "Berliner Zeitung" Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba mradi wa kuijenga shule hiyo ulisimamishwa baada ya kiasi cha dola Milioni nne kutoeka.Na aliehusika na kutoeka kwa fedha hizo ni aliekuwa mkuu wa mradi,Anjimile Mtila-Oponyo yaani dadake Rais wa Malawi Joyce Banda.

Gazeti la"Berliner" linafahamisha katika taarifa yake kwamba ,Anjimile Mtila-Oponyo alifukuzwa kazi na Madonna kutokana na kupotea kwa fedha hizo.Lakini sasa mama huyo ni amelipiza kisasi!

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelev