1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameyazingatia matukio ya nchini Afrika ya Kusini ambapo wafanyakazi wa migodi kadhaa waliuawa na polisi.Pia yameandika juu ya Wachina barani Afrika.

Polisi wakiwashambulia waandamanaji

Polisi wakiwashambulia waandamanaji

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeandika juu ya maafa yaliyotokea nchini Afrika Kusini. Kwa mujibu wa taarifa, wafanyakazi  wa  migodi  zaidi ya 30 waliuawa baada  ya kupigwa risasi na polisi alhamisi iliyopita. Maafa hayo yamesababishwa na mgomo wa wachimba mgodi wa madini ya platinium ambao ni miongoni mwa mikubwa duniani. Gazeti la "Frankfurter  Allgemeine" limeeleza  kwamba "wafanyakazi wa mgodi wa madini ya platinum wa Lonmin wamegoma ili kusisitita madai ya nyongeza za mishahara.Tokea mwishoni mwa wiki iliyopita hali ya hatari imetanda kwenye mgodi wa  Marikana wa madini ya  platinium."

Gazeti  la "Frankfurter Allgemeine" limearifu katika makala yake kwamba polisi wawili na maafisa wa usalama wawili walichomwa visu na kufa. Watu wengine 10 pia waliuawa kutokana na mvutano baina ya polisi  na waandamanaji. Gazeti la "Frankfurt Allgemeine" limeeleza kuwa maafa hayo yamesababishwa pia na mvutano baina ya vyama vya wafanyakazi.

Gazeti la  "Berliner Zeitung"wiki hii linautupia macho uhusiano baina ya China na  nchi za Afrika. Katika makala yake gazeti hilo linasema, China inajifanya rafiki wa Afrika, lakini kuongezeka kwa idadi ya Wachina barani Afrika kunawatia wasi wasi wenyeji wa bara hilo. Gazeti hilo linawaita Wachina kuwa mirija ya kikomunisti, na linaeleza kwamba upinzani dhidi ya wawekaji vitega uchumi na wafanya biashara kutoka China unaongezeka barani Afrika.

"Berliner  Zeitung "linasema kuzidi kuongezeka kwa idadi ya Wachina barani Afrika kunasababisha mikwaruzano baina yao na Waafrika. Mara kwa mara inatokea mivutano baina ya Waafrika na wachina hao."

 Mfano wa hivi karibuni ni matukio yaliyojiri kwenye mgodi mmoja wa makaa ya mawe nchini  Zambia. Wafanyakazi waliokuwa na hasira walimshambulia na kumuua meneja mmoja wa kichina na walimjeruhi mwengine. Wanasiasa na wajumbe wa kibalozi wanafanya  bidii ili mkasa huo ueleweke kama ni uhalifu wa kawaida tu. Lakini kuongezeka kwa matukio ya mvutano baina ya Waafrika na Wachina kunatoa ujumbe mwingine kabisa.

Gazeti la "Berliner Zeitung" limeandika katika taarifa yake kwamba katika nchi ya jirani Zimbabwe, pia yapo matatizo baina ya Waafrika na Wachina. "Berliner Zeitung" linasema Waafrika wanapinga siyo tu mazingira mabaya ya utendaji kazi kwenye kampuni zinazoongozwa na Wachina, bali pia wanalalamika juu ya  idadi kubwa ya wachuuzi kutoka China.

Watoto kadhaa walikutwa kwenye kambi ya siri ya al-Qaeda nchini Somalia.Gazeti la "Bild Zeitung" limechapisha habari hizo. Linasema "watoto hao walikutwa wamefungwa minyororo miguuni, na walikuwa wamejawa hofu machoni. Waligunduliwa baada ya kikosi cha kupambana na ugaidi kuivamia madrasa moja katika mji wa Mogadishu mnamo mwezi wa Julai." Gazeti la "Bild Zeitung" linasema kwamba wataalamu wanakubaliana kuwa watoto hao ambao  wote walikuwa na umri wa chini ya miaka 10 walikuwa wanapewa mafunzo ya kuwa washambuliaji wa kujitoa mhanga.   Kwa mujibu wa gazeti  la "Bild Zeitung" shule hiyo ya Koran ilikuwa  kambi ya siri ya al-Shabaab wanaohusiana kwa ukaribu sana na magaidi wa al-Qaeda.

Gazeti la  "Bild Zeitung" limearifu kuwa watoto hao walipelekwa kwenye kambi hiyo ya al-Shabaab bila ya wazazi wao kujua. Gazeti  hilo limemnukuu mtaalamu wa masuala ya ugaidi, Profesa Peter Neumann, kutoka chuo maarufu cha  King's College cha London akisema kuwa imekuwa inafahamika kwa muda mrefu kwamba al-Shabaab wanawapiga msasa  wa kiitikadi watoto wadogo kama  mtandao wa al-Qaeda unavyofanya.


.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Othman Miraji