1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya Paris na Yola

20 Novemba 2015

Kizazi cha pili na cha tatu cha waafrika kaskazini nchini Ufaransa,Mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram Yola na ndowa ya wake wengi ndizo mada kuu magazetini wiki hii nchini Ujerumani

https://p.dw.com/p/1H9Lu
Mwaasisi wa mashambulio ya kikatili ya Paris Abdelhamid AbaaoudPicha: Reuters/Social Media Website

Mashambulizi ya kigaidi ya Paris yamegubika vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii,sawa na namna yalivyogubika vichwa vya habari vya ripoti za magazeti hayo kuhusu bara la Afrika katika kipindi cha siku saba zilizopita.Sababu kuu ni ule ukweli kwamba takriban waandalizi wote wa mashambulio hayo waliotajwa hadi sasa wana asili ya kiafrika-na hasa Afrika ya kaskazini.Mbali na mashambulio hayo ya Ufaransa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii wameimulika pia Nigeria ambako magaidi wa Boko Haram wanaendelea kuuwa pamoja na madhara na hata faida ya ndowa ya wake wengi.

Tuanzie Ufaransa ambako mashambulio makubwa kabisa ya kigaidi ya Novemba 13 iliyopita-yameangamiza maisha ya watu 129 na zaidi ya 350 kujeruhiwa.Wengi wa waandalizi wa mashambulio hayo ni raia wa Ufaransa na Ubeligiji ambao wazee wao wanatokea Afrika kaskazini.Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linamulika mchango wa Ufaransa barani Afrika na kuandika:"

"Ufaransa ni dola lenye nguvu kubwa kabisa kijeshi barani Afrika-hakuna nchi yoyote nyengine ya Umoja wa Ulaya yenye wanajeshi wengi zaidi,vifaru vingi zaidi na ndege nyingi zaidi za kivita barani humo kama Ufaransa.Zaidi ya wanajeshi 7000 wa Ufaransa,kwa mujibu wa wizara ya ulinzi wanawajibika nchi za nje,;hiyo ni idadi kubwa kabisa ikilinganishwa na wanajeshi 3000 kwa mfano wa Ujerumani wanaowajibika kimataifa.Kimbelembele cha Ufaransa barani Afrika kinatokana zaidi na historia yake kama mtawala wa zamani wa kikoloni.Süddeutsche Zeitung linasema hata baada ya uhuru Ufaransa haijachana na ya zamani,tangu kisiasa,kiuchumi mpaka kijeshi-uhusiano wa Ufaransa na wasomi wa bara hilo ni mkubwa.Hadi wakati huu ilikuwa kwa masilahi ya Ufaransa kuingilia kati mizozo inapozuka katika zile nchi za Afrika zinazozungumza kifaransa na ilikuwa pia kwa masilahi ya nchi shirika za umoja wa ulaya kuiachia Ufaransa uwanja huo tete.Lakini mashambulio ya Novemba 13 huenda yakaibadilisha hali hiyo-linamaliza kuandika gazeti la Süddeutsche Zeitung.

Mashambulio ya kigaidi kaskazini mashariki ya Nigeria

"Yola haiko tena salama" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la mjini Berlin "die Tageszeitung".Ripoti hiyo inazungumzia juu ya shambulio lililotokea kwa mara nyengine tena kaskazini ya Nigeria na kuangamiza safari hii maisha ya watu 32.Mji wa Yola kaskazini mashariki ya Nigeria umelengwa kwa mara nyengine tena-linaandika "Die Tageszeitung" na kumnukuu shahidi akisema mripiko umesikika kilomita kadhaa kutoka mahala bomu lililokoripuliwa.Lengo lilikuwa soko:Sio tu chaguo la mahala bali pia wakati wa kuripuwa bomu hilo ulichaguliwa makusudi ili kuhakikisha watakaouwawa hawatakuwa kidogo.Shambulio hilo limetokea saa za magharibi wakati ambapo watu wengi walikuwa njiani kurejea nyumbani.Hata kama hadi wakati huu hakuna aliyedai kuhusika na shambulio hata hivyo kuna kila dalili limefanywa na kundi la magaidi la Boko Haram.Die Tageszeitung linasema Yola ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Adamawa unalengwa makusudi na Boko Haram kwasababu ya sifa za mji huo za watu wa jamii,makabila na dini tofauti kuishi kwa amani.Gazeti hilo la mjini Berlin linakumbusha hii ni mara ya nne kwa Yola kulengwa na mashambulio ya kigaidi.

Ukewenza una faida zake

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu ndowa ya wake wengi.Gazeti la NZZ am Sonntag linasema ndowa kama hiyo ina faida zake pia.Baada ya kuyanukuu mashirika ya misaada ya maendeleo yanayoelezea athari za umaskini na maradhi yanayoweza kusababishwa na ndowa ya wake wengi,NZZ am Sonntag linasema ndowa ya aina hiyo inaweza pia kumpatia faida mwanamke anapoolewa na mume mwenye wake wengi.Ndowa za wake wengi ni dhulma kwa wake husika na zinaweza kusababisha watoto wengi wanaozaliwa katika ndowa kama hizo kufariki-ni mojawapo ya hoja zinazotolewa mara nyingi kuipinga ndowa kama hizo,lakini gazeti la NZZ am Sonntag limeutaja uchunguzi uliofanywa na wataalam wa London School of Hygien and Tropical Medicine-katika vijiji 56 vya kaskazini mwa Tanzania na kugundua hali inaweza kuwa na faida zaidi kwa wanawake ikiwa watakuwa na uhuru mkubwa zaidi wa kujiamulia mambo yao.Muhimu zaidi ni kuimarisha hali ya kiuchumi katika maeneo husika na kuhakikisha elimu sawa kwa wasichana na wavulana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri:Yusuf Saumu