1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 na masuala muhimu ya Afrika

12 Juni 2015

Afrika katika mkutano wa G7 mjini Elmau, Afrika isonge mbele hadi ifikapo mwaka 2040 na kituo cha kuwalea watoto mjini Nairobi ni miongoni mwa mada za Afrika magazetini nchini Ujerumani wiki hii

https://p.dw.com/p/1FgBm
Kansela Angela Merkel na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika bibi Dlamini Zuma katika mkutano wa kilele wa G7 huko ElmauPicha: picture-alliance/dpa/P. Kneffel

Tuanzie lakini Elmau ulikofanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa saba tajiri kiviwanda G7."Afrika katika safu ya pili" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la Neues Deutschland linalosema Afrika inapozungumziwa basi na mada mfano wa Ebola,Umaskini na ugaidi huwa hazikosekani-lakini pia mada kuhusu ushirikiano wa maendeleo haistahiki kukosekana-linasema gazeti la Neues Deutschland.Tangu miaka kadhaa iliyopitaa limekuwa jambo la kawaida inapoitishwa mikutano kama huu wa viongozi wa mataifa tajiri zaidi kiviwanda duniani,mwandalizi huwachagua na kuwaalika mnamo siku ya mwisho ya mkutano huo baadhi ya viongozi wa Afrika kuketi katika meza ya majadiliano ili kuonyesha kundi hilo la mataifa tajiri zaidi halijifikirii lenyewe tuu na neema zake za kiuchumi,bali wanatilia maanani pia maafa yanawasibu watu masikini zaidi wa dunia hii.Kwa hivyo mkutano wa kilele wa Elmau haukuwa tofauti seuze kansela wa Ujerumani Angela Merkel alilitanguliza mbele tangu mwanzo suala la kupambana na njaa na hali ya ufukara ulimwenguni.Gazeti la Neues Deutschland limekumbusha kile kilichosemwa na waziri wa misaada ya maendeleo wa serikali kuu ya Ujerumani Gerd Müller katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ZDF alipozitaka nchi tajiri kiviwanda G7 ziwajibike zaidi kuelekea bara la Afrika akihoji neema walio nayo inatokana na mali ghafi na hasa kutoka bara la Afrika.

Viongozi wa Afrika watakiwa wawajibike zaidi

Lilikuwa gazeti la Frankfurter Allgemeine lililoandika kuhusu maendeleo barani Afrika:"Afrika inakwenda pole pole".Hadi ifikapo mwaka 2040 linaandika gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine kila kijana mmoja kati ya wawili wa dunia atakuwa anaishi barani Afrika-kwa maneno mengine,nusu ya vijana wa dunia watakuwa wanaishi barani Afrika.Gazeti linasema la muhimu zaidi kuanzia sasa ni kuimarisha elimu na ukuaji wa kiuchumi.Frankfurter Allgemeine limezungumzia mkutano wa viongozi wa kiuchumi wa bara la Afrika uliofanyika mjini Cape Town nchini Afrika kusini-kikao cha mwaka huu kikiadhimisha miaka 25 tangu jumuia hiyo ilipoundwa.Picha ya matumaini mazuri inayojitokeza vikao vya jumuia hiyo vinapoitishwa,imetoweka safari hii,linasema Frankfurter Allgemeine na kumalizia washiriki hawakuchelea kupaza sauti,kuonyesha wasi wasi wao na hata kuzionya serikali zao dhidi ya uhaba wa maendeleo unaoshuhudiwa katika nchi nyingi za bara la Afrika naiwe katika sekta ya miundo mbinu,elimu au afya.Shughuli za kilimo zimetuwama tangu miongo minne iliyopita katika wakati ambapo katika sehemu iliyosalia ya dunia watu wanazungumzia kuhusu "mapinduzi ya kijani".Na licha ya kuenea simu za mkononi barani Afrika,lakini katika teknolojia ya kimambo leo ya habari bara la Afrika bado liko nyuma.Mmoja tu kati ya watu watano barani Afrika ndie anaetumia mtandao-ikilinganishwa na asili mia 80 ya wakaazi wa nchi za jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo barani Ulaya-OECD.

Mfadhili mmojawapo wa Kituo "Tumshangilieni Mtoto,Alfred-Neven-DuMont afariki

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii,inatufikisha jijini Nairobi ambako wakfu wa Alfred -Neven-DuMont unasaidia kugharamia ujenzi wa kituo kipya cha kuwahudumia watoto "Tumshangilieni Mtoto".Mwasisi wa wakfu huo,mchapishaji wa gazeti la jiji la Cologne "Stadt Anzeiger" alikitembelea kituo hicho mwaka jana na kusherehekea pamoja na watoto na wakuu wa kituo hicho Marchi 29 mwaka 2014 miaka 87 ya kuzaliwa kwake.Alfred Neven-DuMont amefariki dunia hivi karibuni na Kölner Stadt Anzeiger likachapisha kumbukumbu za mkuu wa kituo hicho kinachowahudumia watoto kutoka mitaa ya mabanda ya Nairobi,Japhet Njenga.Kölner Stadt Anzeiger limenukuu Japhet Njega akimtaja marehemu Alfred -Neven-DuMont kuwa ni mtu mpole,asiyependa makubwa na aliyekuwa akipigania haki sawa kwa watu maskini na watoto ambao hawakubahatika katika maisha yao.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri: Iddi Ssessanga