1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Josephat Charo21 Desemba 2007

Jacob Zuma achaguliwa kiongozi mpya wa chama cha ANC Afrika Kusini. Kampeni za machafuko nchini Kenya

https://p.dw.com/p/Ceeq
Jacob Zuma baada ya kuchaguliwa kiongozi mpya wa chama cha ANCPicha: AP

Jacob Zuma amechaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama cha ANC nchini Afrika Kusini. Gazeti la Neuer Zürcher Zeitung lilisema wajumbe wa chama cha ANC walimchagua bwana Zuma Jumanne iliyopita kwenye mkutano wa baraza kuu la chama uliofanyika mjini Polokwane. Bwana Zuma alipata ushindi wa wazi kwa kupata kura 2329 dhidi ya rais Thabo Mbeki aliyepata kura 1505.

Kambi ya bwana Zuma katika chama cha ANC inaweza sasa kujiandaa kuchukua cheo cha juu katika chama hicho. Kulikuwa na malumbano kati ya kambi ya bwana Zuma na rais Mbeki kuhusu mfumo wa uliotakiwa kutumiwa kupigia kura huku wafuasi wa Zuma wakitaka kura zihesabiwe kwa mikono wakihofia mfumo wa kutumia kompyuta ungetumiwa kuiba kura.

Mhariri wa gazeti hilo la Neuer Zürcher aliuliza je ushindi wa bwana Zuma ni wa muda mfupi tu? Gazeti lilisema licha ya kukua kwa uchumi, uwekezaji wa kigeni kuongezeka na kupatikana kwa maendeleo katika nyanja mbalimbali nchini Afrika Kuisni chini ya utawalwa rais Thabo Mbeki, wajumbe wa chama cha ANC hawakutaka kumpa zawadi kiongozi huyo kwa ufanisi huo lakini badala yake wakaamu kumuondoa madarakani.

Gazeti la Tagesspiegel lilisema Jacob Zuma sasa anakiongoza chama cha ANC. Ushindi wake dhidi ya rais Thabo Mbeki umezidisha mpasuko ndani ya chama kati ya kambi mbili, moja ya bwana Zuma na ya pili ya rais Mbeki. Sasa ni jukumu la bwana Zuma kuhakikisha pande hizo zinaelewana na kukiunganisha chama cha ANC, jambo ambalo tayari ameahidi kulishughulikia kwa kufanya mazungumzo ya kambi hizo mbili. Mhariri wa Tagesspiegel alisema bwana Zuma ana jukumu la kufanya mashauriano ili kukiunganisha chama cha ANC.

Gazeti la Frankfuurter Allgemeine Zeitung lilimuita Jacob Zuma bwana mkubwa, Big Man, kwa kumshinda rais Thabo Mbeki katika uchaguzi wa chama cha ANC. Nalo gazeti la Neues Deutschland lilisema rais Mbeki alijidanganya mwenyewe akidhani kwa kuwa aligombea uongozi wa chama angeweza kumzuia bwana Zuma kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama.

Kuchaguliwa kwa bwana Zuma kulimaliza mgogoro wa kihistoria uliokuwepo ndani ya chama cha ANC. Mhariri alisema ushindi wa bwana Zuma umemtengenezea barabara ya kwenda ikulu lakini hilo itategemea uamuzi wa mahakama inayomtaka ajibu mashtaka ya rushwa.

Gazeti la Die Welt lilikuwa na kichwa cha maneno kilichosema Zulu- Boy, yaani kijana wa Zulu, sasa ni mtu mwenye mamlaka makubwa zaidi nchini Afrika Kusini. Nchi nzima sasa inasubiri kwa hamu kuona nani atakayekuwa na usemi mkubwa katika chama cha ANC, Je atakuwa bwana Zuma au rais Mbeki, ambao wote wana umri wa miaka 65?

Mada ya pili inahusu uchaguzi nchini Kenya. Gazeti la Neuer Zürcher Zeitung lilisema huku uchaguzi ukikaribia nchini humo kumezuka machafuko ya kikabilia ambayo hayajawahi kuonekana. Wanasiasa wanawashauri wafuasi wao kuua na kuwatandika wafuasi wa vyama vingine katika juhudi za kuwafukuza watu wa makabila mengine kutoka maeneo wanakogombea.

Nalo gazeti la Süddeutsche Zeitung lilisema huku Wakenya wakikaribia kumchagua rais wao mpya, wagombea urais nchini Kenya wanatumia machafuko kati ya makabila mbalimbali ili washinde.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti kuhusu tume ya amani ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Darfur nchini Sudan, UNAMID. Mhariri alisema kiongozi wa tume hiyo, Rodolphe Adada, ameomba msaada kutoka kwa Ujerumani. Ameitaka pia jumuiya ya kimataifa ihakikishe kuna helikopta za kivita na za kusafirishia bidhaa ili kufanikisha kazi ya tume hiyo huko Darfur.

Mada nyingine iliyoripotiwa katika magazeti ya Ujerumani juma hili ni hatua ya wa wanamgambo wa janjaweed nchini Sudan kubadili msimamo wao. Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung lilisema wanamgambo hao sasa wamekuwa adui kwa serikali ya mjini Khartoum kwa sababu wanahisi wamedanganywa, na serikali haiwajali masilahi yao. Wanahofu watapata hasara kubwa wakati vikosi vya Umoja wa Mataifa vitakapoingia katika eneo hilo kuanzia Januari mosi.

Inasemekana kiongozi wa janjaweed, Mohamed Ali Hamiditi, tayari amefanya mazungumzo na kiongozi wa kundi la ukombozi wa Sudan, SLA, Abdelwahid al Nur, kuhusu ushirikiano wa pamoja.