1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Swala kubwa lililozingatiwa na wahariri wa mageti ya Ujerumani juma hili ni vita kati ya majeshi ya Somalia yakisaidiwa na majeshi ya Ethiopia dhidi ya wanamgambo wa mahakama za kiislamu. Chama cha Kijani hapa Ujerumani chautaka Umoja wa Mataifa ujihusishe zaidi katika kuutanzua mzozo wa Darfrur nchini Sudan.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema Marekani inaisaidia Ethiopia ili kuwachakaza wanamgambo wa mahakama za kiislamu nchini Somalia. Kushindwa kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kufikia azimio la pamoja mjini New York katika kikao chake maalumu cha Jumatano usiku hakukupokelewa vizuri na Marekani.

Qatar ilitoa mwito mapigano baina ya pande husika nchini Somalia yakomeshwe mara moja na mazungumzo ya kutafuta amani kati ya serikali ya mpito ya Somalia mjini Baidoa na mahakama za kiislamu mjini Mogadishu yaanzishwe tena. Mwito huo pia ulitaka mataifa yote ya kigeni yakomeshe harakati zao za kijeshi na kuondoka kutoka Somalia.

Nalo gazeti la Süddeutsche Zeitung kuhusu vita nchini Somalia liliripoti juu ya ushindi wa wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia wakisaidiwa na wanajeshi wa Ethiopia kuuteka mjini wa Jowhar na kusonga mbele kilomita 60 karibu na mji mkuu Mogadishu. Kwa mujibu wa walioshuhudia mji wa Mogadishu ulikaribia kutekwa pia kutoka mikononi mwa wanamgambo wa mahakama za kiislamu, lilisema gazeti hilo. Kufutia mapigano hayo viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa nchi za kiarabau walifanya kikao cha dharura mjini Addis Ababa Ethiopia kutafuta njia za kukomesha vita nchini Somalia.

Mhariri alisema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Gonzalo Gallegos, aliashiria mjini Washington kwamba Marekani inaisaidia Ethiopia. Qatar lakini kwa upande wake inapinga vikali kuwepo kwa majeshi ya kigeni nchini Somalia na inataka yaondoke mara moja. Gazeti liliviita vita nchini Somalia kuwa vita vya Marekani barani Afrika.

Gazeti la Tageszeitung lilisema vita vipya kusini mwa Somalia vinawaathiri raia ambao wamekuwa wakikabiliwa na janga moja baada ya lengine. Ukame, vita, mafuriko na sasa vita tena. Kiongozi wa ujumbe wa kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu nchini Somalia, Pascal Hundt, alinukuliwa na gazeti hilo akisema, tunatarajia mamia ya watu kuuwawa katika vita hivi na maelfu ya wakimbizi kulazimika kuyahama makazi yao. Idadi halisi ya watu walioathiriwa katika vita nchini Somalia haijabainika wazi lakini ni wazi kwamba wasomali wengi watateseka kutokana na mapigano hayo.

Pascal Hundt alisema mwaka huu wa 2006 umekuwa mwaka mbaya sana kwa wasomali. Mwanzoni mwa mwaka kulikuwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Baadaye yakaja mapigano mjini Mogadishu. Baada ya miaka 15 hali nchini Somalia ni mbaya na inaendelea kuwa mbaya.

Eneo la kusini ambako majeshi ya Ethiopia yalipambana na wanamgambo wa kiislamu liliathiriwa na mafuriko na kuna uhaba mkubwa wa chakula. Wasomali takriban milioni 1,1 wanakabiliwa na njaa nusu kati yao kwa sababu ya mafuriko. Raia hawakuwa na nafasi ya kupanda mazao yao kati ya mwezi Oktoba na Disemba kwa sababu ya mafuriko na mapigano. Bei za chakula zimepanda na sio wengi walio na fedha za kununulia chakula.

Likitubadilishia mada gazeti la Süddeutsche liliripoti kuhusu hatua ya chama cha Kijani hapa Ujerumani kuutaka Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani ijihusishe zaidi katika kuutanzua mzozo wa Darfur nchini Sudan. Msemaji wa sera ya kigeni wa chama cha Kijani, Kerstin Müller, amenukuliwa na gazeti hilo akisema angetaka Ujerumani ishiriki katika juhudi za kurejesha amani Darfur. Ujerumani haiwezi kukaa kando katika juhudi za kukomesha mauaji ya halaiki, alisema Kersten Müller, na kupendekeza Ujerumani itume wanajeshi wake kwenda Darfur kushiriki katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatukamilishia na habari za kutengezwa mbuga kubwa ya tembo itakayoziunganisha Angola, Zambia, Zimbabwe, Namibia na Botswana. Mbuga hiyo itakuwa na ukubwa kama wa Italia. Na kufikia hapo ndio nakamilisha Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili.

 • Tarehe 29.12.2006
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHU6
 • Tarehe 29.12.2006
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHU6