1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON: Congo Brazzaville yapata ushindi

22 Januari 2015

Michuano ya kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika iliingia katika siku yake ya 5 huko Guinea ya Ikweta ambapo Congo iliibwaga Gabon na Burkina Faso ikatoka sare na wenyeji Guinea ya Ikweta.

https://p.dw.com/p/1EOnC
Fußball Afrika Cup of Nations Kongo vs. Gabon 21.01.2015
Wachezaji wa Congo wakifurahia bao laoPicha: AFP/Getty Images/C. de Souza

Congo Brazzaville ilisherehekea usiku wake wa kihistoria katika mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika nchini Guinea ya Ikweta jana Jumatano(21.01.2015) wakati Burkina faso ambayo ni makamu bingwa wa kombe hilo walishuhudia matumaini yao ya kufika angalau katika awamu ya mtoano ya timu nane yakivurugika kwa kiasi kikubwa.

Afrika Cup Kongo vs Gabun 21.01.2015
Mpambano kati ya Congo na GabonPicha: K. Desouki/AFP/Getty Images

Congo ilipata ushindi wake wa kwanza katika fainali hizi katika muda wa zaidi ya miongo minne, wakiishinda Gabon kwa bao 1-0 lililopachikwa wavuni na Prince Oniangue na kukaribia kukata tikiti yake katika duru ijayo ya mtoano kutoka kundi A.

Hapo mapema , katika kundi hilo la A, wenyeji Guinea ya Ikweta iliwalazimisha Burkina Faso kwenda sare ya bila kufungana na kuweka matumaini ya timu hizo katika mizani.

Kocha afurahishwa na timu yake

Ilikuwa ni jioni ya kukatisha tamaa kwa Gabon, ambayo ilikuwa inafahamu kwamba ushindi dhidi ya kikosi cha Claude Le Roy , Congo ungewapeleka moja kwa moja katika duru ya robo fainali wakiwa bado na mchezo mmoja kibindoni, lakini walijutia majaliwa yao kutokana na kukosa nafasi kadhaa.

Fußball Afrika Cup of Nations Kongo vs. Gabon 21.01.2015
Prince Oniangue mfungaji wa bao pekee la CongoPicha: REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Congo iliweza kuhimili vishindo hadi mapumziko na baada ya hapo ilipata fursa dakika tatu baada ya kuanza kipinfi cha pili wakati Oniangue alipopachika mpira wavuni baada ya safu ya ulinzi ya Gabon kushindwa kuuondoa mpira wa kona.

Gabon ilipoteza nafasi kadhaa za wazi za kusawazisha katikati ya kipindi hicho wakati Bulot, kutoka klabu ya Charlton Athletic ya Uingereza, alipouelekeza mpira nje kidogo ya goli wakati mlango ulikuwa wazi hauna mlinzi.

Congo ililinda vizuri ushindi wake wa kwanza katika kinyang'anyiro cha fainali za kombe la mataifa ya Afrika tangu ilipofanikiwa kuingia katika nusu fainali nchini Misri mwaka 1974, na kusababisha kocha wao mzoefu raia wa ufaransa Le Roy kuwamiminia sifa tele wachezaji wake.

"Sijapata kuwa na timu ambayo inafanyakazi vizuri kimbinu kama hii, hata kama tunamakosa katika baadhi ya sehemu," amesema Le Roy, ambaye anajitokeza kwa marab yake ya nane katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika kama kocha.

Kikosi chake sasa kinahitaji pointi moja dhidi ya Burkina Faso katika mchezo wake wa mwisho katika kundi A siku ya Jumapili ili kuweza kujihakikishia nafasi katika robo fainali, lakini Le Roy anasisitiza wataingia uwanjani kupata ushindi.

Fußball Afrika Cup of Nations Äquatorialguinea vs. Burkina Faso
Mashabiki wa Burkina FasoPicha: AFP/Getty Images/K. Desouki

"Nilikuwa mshambuliaji katika enzi zangu, mimi si kocha hodari duniani kucheza kwa kutafuta sare. Iwapo tutaingia dimbani kutafuta sare, nastahili kufukuzwa kazi mara moja." Amesema.

Bahati yawatupa mkono Gabon

Wakati huo huo kocha wa Gabon ambae amebaki ameduwaa Jorge Costa amesema: "Tulipata nafasi katika kipindi cha kwanza lakini bahati ambayo tuliipata dhidi ya Burkina Faso haikuwapo leo."

Burkina Faso pia ilipoteza mchezo wake wa kwanza kwa mabao 2-0 dhidi ya gabon siku ya Jumamosi ya ufunguzi wa mashindano haya baada ya kushindwa kutumia fursa ilizopata na walibakia wakijutia na kushindwa kuweka mpira wavuni.

Sambia Fußball Nationalmannschaft
Kikosi cha Zambia , ChipolopoloPicha: P. Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Leo jioni (22.01.2015)Zambia itajitupa uwanjani kupambana na Tunisia na Cape Verde ina miadi na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo katika michezo ya kundi B.

Na kwa taarifa hiyo ya michezo ndio tumehitimisha uchambuzi wetu wa taarifa za uchunguzi kutoka hapa na pale ulimwenguni. Manaendelea kusikiliza Dunia Yetu Leo jioni kutoka Dw Bonn.

Mwandishi: Mohamed Dahman

Mhariri: Iddi Ssessanga