1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA: Wito kwa Zimbabwe kuheshimu haki za binadamu

17 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCI3

Umoja wa Afrika leo umetoa wito kwa Zimbabwe kuheshimu haki za binadamu na misingi ya udemokrasia.Hayo ni matamshi makali kabisa kupata kutolewa na umoja huo kuhusika na mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe.Kamishna mkuu wa Umoja wa Afrika,Alpha Oumar Konare amesema,umoja huo wenye wanachama 53,unatazama matokeo ya nchini Zimbabwe kwa wasiwasi mkubwa.Kwa upande mwingine,Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe,amepuuza lawama za jumuiya ya kimataifa zilizochochewa na picha zilizomuonyesha kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai akiwa na majeraha mabaya.Tsvangirai aliekamatwa siku ya Jumapili pamoja na wafuasi wa upinzani darzeni kadhaa walipokuwa njiani kwenda kuhudhuria mkutano wa kumpinga Mugabe,amesema alipigwa vibaya sana alipokuwa mikononi mwa polisi.Desmond Tutu wa Afrika ya Kusini alietunukiwa zawadi ya amani ya Nobel amesema viongozi wa Kiafrika wanapaswa kuona aibu kuhusu mgogoro wa Zimbabwe.Amesema,viongozi hao wakimsifu Mugabe na wakishikilia kuwa wanaheshimu uhuru wake,wamewavunja moyo Wazimbabwe,mara nyingi sana.