1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Accra. Mvua kubwa zasababisha maafa barani Afrika.

19 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBOR

Watabiri wa hali ya hewa wanatabiri kuwa mvua zaidi zitanyesha katika sehemu kubwa ya bara la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ambako mafuriko makubwa kuwahi kutokea katika muda wa miaka 30 yamesababisha watu 270 kupoteza maisha katika wiki za hivi karibuni.

Umoja wa mataifa na shirika la kutoa misaada la msalaba mwekundu limesema wahanga wengi wamepoteza maisha kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji kama kuharisha. Wameanzisha miito ya kupatiwa fedha za kuwasaidia watu zaidi ya milioni moja katika mataifa 17 ya Afrika. Moja kati ya nchi ambazo zimeathirika mno ni Sudan , ambako watu 64 wamefariki kutokana na mafuriko na watu 49 wamefariki kutokana na ugonjwa wa kipindupindu.Nchini Ghana kumetokea vifo 32 hadi sasa. Nchini Uganda mafuriko yamewalazimisha watu 50,000 kukimbia makaazi yao katika jimbo la mashariki la Teso. Kiasi cha watu 300,000 wanategemea chakula cha msaada tu. Burkina Faso na Togo pia zimeathirika na hali hiyo mbaya ya hewa. Mashirika ya kutoa misaada yamesema mvua imeharibu mazao, hususan nchini Ghana. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imesema kuwa msaada wake kwa wahanga wa mafuriko katika bara la Afrika umeongezwa kwa kiasi cha Euro 430,000.