1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abuja. Viongozi wa ECOWAS washindwa kukwamua mkwamo wa kisiasa Ivory Coast.

7 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD5J

Viongozi wa mataifa ya Afrika magharibi wamekutana jana Ijumaa kujaribu kuzibua mkwamo katika nchi ya Ivory Coast ambayo imegawanyika kutokana na vita, lakini wameamua badala yake kuuachia umoja wa mataifa kuamua kile kitakachofuatia baada ya rais Laurent Gbagbo muda wake ambao tayari umerefushwa utakapomalizika hapo mwishoni mwa mwezi huu.

Gbagbo, ambaye alinusurika jaribio la kuipindua serikali yake mwaka 2002 na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuiacha nchi hiyo ikigawanyika , alikuwa anatarajiwa kutayarisha uchaguzi ambao umeahirishwa kwa muda mrefu kabla ya Oktoba 31, wakati ambapo muda wake wa mwaka mmoja zaidi aliyoongezewa madarakani unamalizika.

Katibu mtendaji wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS, Mohammed ibn Chambas amesema kuwa mapendekezo yaliyojadiliwa katika mkutano huo yatawasilishwa katika mkutano wa umoja wa Afrika baadaye mwezi huu kabla ya kupelekwa katika umoja wa mataifa.