1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abidjan: Viongozi wa Afrika na Ulaya wakutana kuhusu ajira

Mohammed Abdul-Rahman29 Novemba 2017

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Afrika wakutana katika mkutano wa kilele mjini Abidjan kushajiisha juu ya ajira na utulivu

https://p.dw.com/p/2oRdh
Mittelmmeer gerettete afrikanische Flüchtlinge
Picha: picture-alliance/AP/E. Morenatti

Zaidi ya viongozi 80 wa Afrika na Ulaya wanakusanyika mjini Abidjan-Cote d´Ivoire leo, kushajiisha juu ya ajira na utulivu kwa  idadi inayozidi kuongezeka barani  Afrika, huku baadhi wakitoa wito wa kuwepo mpango mpya wa  uokozi sawa na ule uliobuniwa  kuisaidia Ujerumani baada ya  vita unaojulikana kama " Mpango wa Marshall."

Mkutano huo wa siku mbili mjini Abidjan unafunguliwa wakati Umoja wa Ulaya ukizidi kuona hatima yake ikifungamana na  Afrika, kufuatia  matukio mawili yasiotarajiwa-uhamiaji na  mashambulizi ya kigaidi. Unafanyika wakati China, India, Japan na mataifa ya ghuba na  mengineyo pia yakiwania ushawishi barani humo, ambako mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya kwa jumla yakisalia kuwa  nguzo muhimu ya kiuchumi na kisiasa .

Mamilioni ya nafasi za ajira zahitajika Afrika

Rais wa bunge la Ulaya Antonio Tajani amesema Afrika inapaswa kuunda mamilioni ya nafasi za ajira kukabiliana na idadi mpya ya watu wake
Rais wa bunge la Ulaya Antonio Tajani amesema Afrika inapaswa kuunda mamilioni ya nafasi za ajira kukabiliana na idadi mpya ya watu wakePicha: European Union 2017 - Source : EP

Rais wa bunge la Ulaya mwanasiasa wa Italia  Antonio Tajani aliwaambia wabunge kutoka abara yote mawili kabla ya mkutano huo wa kilele kwamba  kuna muda mdogo mno wa kutafuta njia  ya kuweza kukidhi mahitaji ya  umma wa Afrika, ambao idadi yao  itaongezeka maradufu ifikapo 2050 na kufikia watu bilioni 2.4. Tajani alisema Afrika inapaswa kuunda mamilioni ya nafasi za ajira kukabiliana na idadi mpya ya watu wake katika soko la ajira na kwamba ikiwa hilo halitatokea vijana watapoteza matumaini.

Akizungumza na  DW kabla ya mkutano kwenye mji  huo wa kiuchumi wa Cote d´Ivoire  kuhusu hali ya  vijana barani Afrika kuwa sawa na Bomu na  ikiwa anafikiria viongozi wenzake kweli wanalielewa hilo,  Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais  Alpha Conde wa Guinea alisema:-

" Nimeyasema haya miaka minne sasa. Kuna haja  ya kuwekeza kwa vijana  kwa hiyo viongozi wote  wa  Afrika wanazingatia  kwamba vijana  vijana ndiyo matumaini yetu na pindi hakutakuweko na ajira  kwa vijana , Afrika italipuka. Kwa  hiyo viongozi wanaelewe juu ya haja ya kupambana na rushwa, kuekreza kwa vijana  na  utawala bora."

Mabilioni ya Euro kukuza maendeleo ya kiuchumi Afrika yatengwa

Mkutano huo huenda pia ukazungumzia  matukio ya kushtusha ya wahamiaji  wakiuzwa kama watumwa nchini Libya
Mkutano huo huenda pia ukazungumzia  matukio ya kushtusha ya wahamiaji  wakiuzwa kama watumwa nchini LibyaPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Umoja wa Ulaya  umetenga mfuko wa mabilioni ya Euro kukuza maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, wakati ukitanua zaidi ushirikiano na nchi za kiafrika katika kupambana na  ugaidi katika bara hilo ambako makundi ya kiislamu ya siasa kali yanajitanua.

Balozi wa Morocco katika Umoja wa ulaya  Ahmed Reda Chami pia ametoa wito wa kuwepoo mpango wa Marshall kwa ajili ya Afrika, lakini utakaolindwa na hatua dhidi ya rushwa na kuzingatia  mahitaji ya Afrika.  Itakumbukwa mpango wa Marshall wa mabilioni ya dola ulianzishwa na Marekani baada ya vita vya pili ya dunia, kulisaidia bara Ulaya kujikwamua kiuchumi na kuweza kufikia mafanikio makubwa na utulivu unaoshuhudiwa hii leo.

Mkutano huo wa kilele wa mataifa 55 ya  Umoja wa  Afrika na 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya  huenda pia ukazungumzia  matukio ya kushtusha ya wahamiaji kupigwa mnada huku wakiuzwa kama watumwa nchini Libya . Rais wa halmashauri  kuu ya Umoja wa Afriaka  Moussa  Faki Mahamat ametoa wito wa kuchuliwa hatua za dharura kuzuwia mtindo huo, ambao wakosoaji wanasema umetokana na  kushindwa kuwepo kwa ushirikiano wa kutosha kuzuwia wimbi la wahamiaji wenye kiu cha kuingia barani Uaya kwa kupitia Libya.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp

Mhariri:Josephat Charo