1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abdullah Gul ameshindwa duru ya pili

P.Martin24 Agosti 2007

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki,Abdullah Gul hii leo kwa mara nyingine tena,ameshindwa kupata kura za kutosha katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais.

https://p.dw.com/p/CH96
Waziri wa Nje wa Uturuki,Abdullah Gul pamoja na mkewe Haryunisa
Waziri wa Nje wa Uturuki,Abdullah Gul pamoja na mkewe HaryunisaPicha: picture-alliance/dpa

Gul ni mwanadiplomasia anaeheshimiwa sana na alitoa mchango mkubwa kusaidia kuanzishwa kwa majadiliano ya uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya.Lakini,kwa sababu ya kuwahi kuwa waziri katika serikali iliyoongozwa na chama cha Kiislamu na kutimuliwa mwaka 1997,Gul haaminiwi na kundi la wasomi,ikiwa ni pamoja na majemadari wa kijeshi,viongozi wa upinzani na majaji.

Uturuki yenye wakazi wapatao milioni 74,ni nchi yenye Waislamu wengi lakini inaongozwa na katiba isiyoingiza dini katika masuala ya kisiasa.Chama tawala cha AK chenye mizizi ya Kiislamu, kinatuhumiwa kuwa kinajaribu kupuuza utaratibu huo wa kutenganisha dini na siasa,ambao ulianzishwa baada ya kuporomoka kwa ufalme wa Ottoman na ikaundwa jamhuri mpya ya Uturuki.

Lakini chama cha AK kinakanusha tuhuma hizo na kinakumbusha mageuzi yaliyofanywa na serikali hiyo kama ilivyopendekezwa na Umoja wa Ulaya pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya biashara tangu serikali hiyo kushika madaraka.

Ni wachache wanaoamini kuwa jeshi lililowahi kupindua serikali nne tangu mwaka 1960,litachukua hatua ya moja kwa moja,baada ya kudhihirika kuwa matamshi makali yaliyotolewa na wanajeshi mapema mwaka huu,yalisaidia kukipatia chama cha AK kura nyingi zaidi katika chaguzi za bunge.

Kushindwa kuchaguliwa kwa Gul mapema mwaka huu, kulisababisha kuitishwa chaguzi mpya za bunge na chama cha AK kilijinyakulia ushindi mkubwa.

Ikiwa Abdullah Gul atashinda katika duru ya tatu,kama inavyotazamiwa,basi wadhifa wa urais, kwa mara ya kwanza katika historia mpya ya Uturuki,utashikwa na mfuasi wa zamani wa chama cha Kiislamu.

Uturuki,rais ana kura ya turufu na huweza kupinga sheria na maafisa wanaoteuliwa.Vile vile ana mamlaka ya kuwateua majaji.Wadhifa huo una uzito mkubwa wa maadili kwa sababu,mara ya kwanza kabisa,ulishikwa na muasisi wa nchi hiyo,Mustafa Kemal Ataturk ambae hakuchanganyisha masuala ya dini na siasa.