1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abdullah al-Senussi akamatwa

MjahidA18 Machi 2012

Serikali nchini Mauritania imesema imemkamata mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi wa aliyekuwa kiongozi wa Libya hayati Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/14MIW
Mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi nchini Libya Abdullah Al-Senussi
Mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi nchini Libya Abdullah Al-SenussiPicha: dapd

Abdullah al-Senussi alikamatwa wakati alipowasili mjini Nouakchott kwa ndege iliokuwa imetoka Casablanca, Morocco akiwa na hati bandia ya usafiri.

Senussi anatakiwa na mahakama ya uhalifu wa kivita ya The Hague ilioko uholanzi, kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu wakati wa machafuko ya mwaka uliopita nchini Libya. Ofisi ya rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy imesema kuwa Ufaransa imesaidia katika kukamatwa kwa Senussi na kutaka pia apelekwe nchini humo ili ashtakiwe kwa makosa aliodaiwa kutekeleza, wakati wa ulipuaji wa ndege moja mwaka wa 1989 nchini Niger iliosababisha vifo vya raia 54 wa Ufaransa.

Mahakama ya uhalifu wa kivita ICC pia inataka Abdullah al-Senussi apelekwe katika mahakama hiyo ili kujibu mashtaka ya kuhusika na mauaji ya zaidi ya wafungwa 1,200 katika gereza la Abu Salim mjini Tripoli mwaka wa 1996. Msemaji wa mahakama ya ICC amesema waranti ya kumkamata Senussi bado ipo na kuomba itekelezwe.

Majaji katika Mahakama ya ICC mjini Hague, Uholanzi
Majaji katika Mahakama ya ICC mjini Hague, UholanziPicha: AP

Hata hivyo msemaji wa utawala mpya wa Libya Nasser al-Manee akizungumza na wanahabari mjini Tripoli amethibitisha kukamatwa kwa Abdullah al-Senussi, pamoja na kijana mdogo anayedhaniwa kuwa mwanawe. Kulingana na msemaji wa baraza la kitaifa la mpito Libya Mohammed al-Harizy wanafanya mipango ya kumrejesha mhalifu huyo wa kivita nchini humo ili afunguliwe mashtaka.

Lazima Senussi akabidhiwe ICC

Kwa upande wake shirika la kutetea haki za kibinaadamu la Amnesty International limesema lazima mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi Abdullah Senussi akabidhiwe kwa mahakama ya ICC kujibu mashtaka yanayomkabili.

Kaimu mkurugenzi wa shirika hilo anayesimamia Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Hassiba Hadj Sahraoui, amesema utawala wa Mauritania unapaswa kuipa kipaumbele waranti ya kukamatwa kwa Al Senussi iliotolewa na mahakama hiyo Juni 27 na kumkabidhi huko haraka ili ajibu mashtaka anayokabiliwa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mwandishi Amina Abubakar/RTRE

Mhariri Sekione Kitojo