1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abdel Aziz ashinda uchaguzi Mauritania.

Halima Nyanza20 Julai 2009

Serikali nchini Mauritania imesema Jenerali Mohamed Ould Abdel Aziz, ambaye alimpindua rais wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia katika mapinduzi yaliyotokea mwaka jana, ameshinda uchaguzi wa Rais.

https://p.dw.com/p/Iswi
Jenerali Mohamed Ould Abdel Aziz, ameshinda uchaguzi wa Rais nchini Mauritania.Picha: dpa

Akitangaza matokeo hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Mauritania, Mohamed Ould Rzeizim, amesema Abdel Aziz ameshinda kwa asilimia 52.6 ya kura zote zilizopigwa.


Amesema hakuna malalamiko yoyote rasmi yaliyotolewa kuhusu matokeo hayo na kuondoa haja ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi.


Muda mchache kabla ya Waziri wa Mambo ya Ndani kutangaza matokeo hayo, wapinzani walipinga uchaguzi huo kwa kuiita kuwa ni wa kinafiki.


Kwa upande wake, Mohamed Ould Biya, msemaji wa kundi hilo, ameelezea kufanyika kwa udangamnyifu katika uchaguzi huo kwa kusema kuwa orodha ya wapiga kura ilivurugwa na wapiga kura walitumia karatasi za kupiga kura za uwongo na vitambulisho wakati wa zoezi hilo ili kumuwezesha Jenerali Abdel Aziz ashinde.


Wagombea wa upinzani wametoa wito kwa jumuia ya Kimataifa kufanyika uchunguzi wa madai hayo ya kufanyika kwa hila.


Akielezea ushindi wake, Jenerali Jeneral Abdel Aziz amesema ushindi humo ni mapambano dhidi ya Umasikini na ujinga na kuongeza kuwa wale wote wanaosema kwamba udanyanyifu umefanyika katika uchaguzi huo wawasilishe malalamiko yao wakiwa na ushahidi kamili.


Ameahidi pia kupambana na ugaidi katika nchi hiyo ambayo pia imekuwa ikikumbwa na mashambulio ya hapa na pale yanayofanywa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, ambapo siku moja kabla ya uchaguzi polisi nchini humo walipambana na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Al Qaeda katika mji mkuu wa nchi hiyo, wiki moja baada ya kundi moja kudai kumuua mfanya kazi wa misaada wa Kimarekani.


Jenerali Abdel Aziz amesema nchi yake imekuwa ikikabiliwa na vitisho vya ugaidi kwa kiwango cha juu na kusema kwamba wanahitaji kupambana na ugaidi sio tu kwa kuimarisha ulinzi, lakini pia kuimarisha hali za watu katika kupambana na ujinga.



Uchaguzi huo wa Urais uliofanyika siku ya jumamosi ulikuwa ni wa kwanza tangu Jenerali Abdel Aziz alipomuondoa madarakani Rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia katika nchi hiyo ya Kiislamu mwaka jana mwezi uliopita.


Uchaguzi huo unaonesha wawekezaji na wafadhili kwamba nchi hiyo iko tayari kujiunga tena na jumuia ya kimataifa baada ya vikwazo vilivyowekwa kama adhabu baada ya kufanyika kwa mapinduzi hayo.


Katika uchaguzi huo hakujatumwa waangalizi kutoka Umoja wa Mataifa wala Umoja wa Ulaya ambazo zimekata misaada yeke kwa nchi hiyo.



Mwandishi: Halima Nyanza Reuters/AP

Mhariri: Miraji Othman