1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

40,000 wandamana kumpinga Breivik Norway

Admin.WagnerD26 Aprili 2012

Maelfu ya raia wa Norway siku ya Alhamis walifanya mandamano makubwa mjini Oslo huku wakiimba wimbo wa watoto wa Kole - We're the Children of the Rainbow ambao unamchukiza sana katili Anders Behring Breivik.

https://p.dw.com/p/14lVF
Wandamanaji wakiwa katika uwanja wa Youngstortget.
Wandamanaji wakiwa katika uwanja wa Youngstortget.Picha: dapd

Wakiitikia wito uliotolewa kupitia mtandao wa intanet, takribani wandamanaji elfu 40 wamekusanyika katika viwanja vya Youngstort wakiwa wamevalia makoti ya nvua na kubeba bendera za Norway na maua, ambavyo vimekuja kuwakilisha mwitiko wa amani wa nchi hiyo kwa mashambulizi hayo ya kikatili.

Breivik, mwenye itikadi kali ya mrengo wa kulia, anauchukulia wimbo huo kama kasumba ya mfumo wa umaksi. Breivik aliiambia mahakama Ijumaa iliyopita kuwa Nilsen ni mfano mzuri wa mmaksi aliyejipenyeza katika mandhari ya utamaduni na kwamba wimbo wake umewatia kasumba wanafunzi wa Norway.

Baadhi ya watu waliohudhuria kesi ya Breivik.
Baadhi ya watu waliohudhuria kesi ya Breivik.Picha: Reuters

Nchi za Skandinavia zaunga mkono
Mawaziri wa utamaduni wa nchi za Skandinavia nao walikuwepo katika uwanja huu kushiriki shughuli hii ambapo wanadamanaji walikuwa wanatembea pamoja kwa taratibu huku wakiimba huo wa We're the children of the rain bow wa msanii Lillebjoern Nilsen unaomaanisha kuwa sisi ni watoto wa tamaduni mbalimbali. Nilsen alikuwa akiongoza kiitikio cha wimbo huu huku umati uliohusisha pia watoto wa shule za msingi wakifuatisha na kupunga maua hewani.

Kufuatia matamshi haya ya Breivik kuhusu wimbo huo na Nilsen, raia wawili wa Norway walianzisha kampeni kupitia mtandao wa facebook wakiwataka wa Norway kuthibitisha hadhi ya wimbo huo kwa kuuimba pamoja mbele ya chumba cha mahakama.

Wimbo wa Children of the Rainbow ni marekebisho ya wimbo wa 'My Rainbow Race' wa msanii wa muziki wa jadi kutoka Marekani Pete Seeger, na ni maarufu sana katika nchi ya Norway. Kiitikio chake kinasema: Pamoja tutaishi, kila kaka na kila dada, watoto wadogo wa kole, na dunia ya kijani.

Marie Naess na Aashild Nestdgaard wakifunga maufa nje ya chumba cha mahakama kuwakumbuka wahanga
Marie Naess na Aashild Nestdgaard wakifunga maufa nje ya chumba cha mahakama kuwakumbuka wahangaPicha: Reuters

Muathirika wa kwanza atoa ushahidi
Wakati huo huo, muathirika wa kwanza wa bomu lililotegwa na Breivik katika jengo la serikali tarehe 22 Julai 2011, Eivind Dahl Thoresen alitoa ushahidi mahakamani siku ya Alhamis na kusema:

"Ni kama kumbukumbu ya filamu mbaya. Nakumbuka sana nilivyostushwa na mlipuko mkubwa ambao ulinirusha nyuma kwa mita nyingi."

Madaktari wanasema Eivind alikuwa ni mwenye bahati kupata watu wa kumsaidia kumuwahisha matibabu. Akielezea hali baada ya kuzinduka, Eivind anasema:

"Nilizinduka, niliona mwanaume wa makamo akiwa karibu yangu akililia msaada. Nilifikiri kwanza kuwa mimi nimesalimika na hivyo napaswa kumsaidia. Lakini baada ya kujiangalia niliona mwili wangu wote umejaa damu nikaamua nitulie niite watu wa kunisaidia."

Breivik akiteta na wakili wake Vibeke Hein Baera mahakamáni.
Breivik akiteta na wakili wake Vibeke Hein Baera mahakamáni.Picha: picture-alliance/dpa

Eivind, mwenye umri wa miaka 26 amesema hivi sasa anajaribu kurudia maisha yake kama ilivyokuwa huko nyuma ingawa wataalamu wanasema itamchukulia muda mrefu kutokana na ukweli kuwa baadhi ya viungo vyake vilioza.

Breivik anakiri kufanya mashambulizi mawili yaliyosababisha vifo vya watu 77, lakini anakanusha kuwa na hatia kwa madai kuwa ingawa yalikuwa mashambulizi ya kikatili, yalikuwa muhimu kukizuia chama tawala nchini humo cha wafanyakazi kuruhusu utamaduni mchanganyiko na ongezeko la Waislamu nchini Norway na Ulaya kwa ujumla.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman