| Habari za Ulimwengu | DW | 16.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

ANKARA: Wagombea wajiandikisha

Hekaheka za uchaguzi wa Urais nchini Uturuki zimeanza baada hii leo, huku wagombea wa nafasi hiyo wakianza kujiandikisha.

Uandikishaji wa wagombea umekuja baada ya maandamano ya mwisho wa wiki kupinga hatua ya chama tawala kupendekeza Waziri mkuu wa nchi hiyo Tayyip Erdogan kuwa mgombea wake.

Karibu watu laki 3 waliingia mitaani katika mjini Ankara wakitaka dini na siasa kutenganishwa.

Wakosoaji wanasema Erdogan anaunga mkono kuhusisha uislam katika siasa za Uturuki, hartua ambayo huenda ikatishia nyanja za siasa ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa sheria ya sasa ya Uturuki , Rais anaweza kubadili sheria, kuteua maafisa wengi muhimu katika serikali na kuwa amiri jeshi mkuu.

Duru ya pili ya uandikishaji wa wabunge imepangwa kuanza wiki ijayo.

BERLIN-Ujerumani yaishutumu Russia

Ujerumani imeishutumu Russia kufuatia vikosi vya usalama nchini humo kuwashambulia waandamanaji wanaoipinga serikali.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Ujerumani utumiaji mkubwa wa nguvu uliokithiri wa vyombo vya usalama nchini Russia unahatarisha maendeleo ya nchi hiyo.

Mwishoni mwa wiki hii katika viwanja vya mtakatifu Petersburg Polisi waliwapiga na kuwatia ndani mamia ya waandamanaji waliokusanyika katika miji miwili nchini humo kupinga ukiukwaji wa demokrasia unaofanywa na serikali ya Rais Vladimir Putin.

Baadhi ya waandishi wa habari wa Ujerumani ni miongoni mwa watu waliokamatwa.

KABUL-Polisi wanane wauawa

Polisi wanane wameuawa nchini Afghanstan kufuatia shambulio la bomu la kujitoa muhanga katika kituo cha mafunzo cha jeshi la Polisi katika mji wa kaskazini wa Kunduz.

Hivi karibuni kundi la Taliban lilianzisha mashambulio kadhaa ya kigaidi katika miji ya kusini na mashariki, ingawa ni mara chache mashambulizi hayo kutokea maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo ambapo jumla ya wanajeshi 3,000 wa Ujerumani wamepiga kambi.

Wakati huo huo shirika la haki za binaadam la New York limesema vifo vinavyotokana na mashambulizi ya ugaidi nchini Afghanstan vimeongezeka ndani ya miezi 15.

Katika ripoti yake shirika hilo limesema karibu raia 700 wameuawa kufuatia mashambulio katika kipindi hiki toka kundi la Taliban lilipoondoshwa madarakani na majeshi ya Marekani na yale ya muungano miaka sita iliyopita.

BAGHDAD-Kundi la Sadr lajitoa serikalini Iraq.

Kundi la madhehebu ya shia la Moqtadar Al Sadr limesema limejiondoa katika serikali ya muungano nchini Iraq, baada ya Waziri mkuu wa nchi hiyo Nuri Al Malk kukataa kupanga ratiba ya kuondoa majeshi ya Marekani.

Kundi hilo lenye ushawishi mkubwa miongoni mwa washia walio wengi nchini Iraq, limewaondoa mawaziri wake sita huku likishikilia msimamo wa kuyataka majeshi ya Marekani kuondoka nchini humo.

Mmoja wa wabunge wa chama cha Sadr Baha Al Avaji amesema sheria hiyo itaangaliwa na kupelekwa mbele ya Umoja wa mataifa na Marekani.

Hatua hiyo imekuja baada ya ghasia za mwisho wa wiki iliyopita ambapo jumla ya watu 43 waliuawa mjini Baghdad kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Katika shambulio hilo jumla ya watu 160 walijeruhiwa.

Kundi la Sadr linahusishwa na matukio kadhaa ya mauaji nchini Iraq ,likishikilia msimamo wake wa kuondoa majeshi ya kigeni nchini humo, toka utawala wa Rais wa zamani wa nchi hiyo Marehemu Saddam Hussein ulipoangushwa miaka minne iliyopita.

KHARTOUM-Sudan yakubali mapendekezo ya UN

Serikali ya Sudan imesema imekubali mapendekezo yote ya baraza la usalama la umoja wa mataifa ikiwamo matumizi ya helikopta za kijeshi katika eneo la Darfur.

Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Lam Akol amesema Serikali ya Sudan imekubali awamu ya pili ya makubaliano na umoja wa mataifa kuyasaidia majeshi ya umoja wa Afrika nchini humo.

Hii leo Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ba Ki Moon anafanya mazungumzo ya pamoja na Katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiafrika Omar Alpha Konare juu ya upelekwaji wa vikosi vya kulinda amani nchini Sudan.

Akihitimisha ziara yake ya siku tatzu nchini humo , naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Negroponte mapema leo amesema nchi yake itachukua hatua iwapo Sudan haitakubali kutekeleza mapendekezo ya Baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Marekani amesema kwa hali aliyoiona ni dhahiri kuwa serikali ya Sudan inalisaidia kundi la Janjaweed linaloendesha mauaji katika eneo la Darfur.

ABUJA-Mahakama yaamuru atiku kugombea Urais

Mahakama kuu ya Nigeria imeamuru mgombea wa kiti cha urais nchini humo bwana Atiku Aboubakar kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi wa jumamosi.

Bwana Atiku ambaye ni makamu wa Rais wa nchi hiyo amefunguliwa mashtaka ya rushwa na tume ya uchunguzi wa makosa ya uchumi na fedha ya nchi hiyo.

Hatua hiyo ilipelekea tume ya uchaguzi nchini humo kumsimamisha Bwana Atiku kugombea kiti cha urais mapema mwezi huu.

Mahakama hiyo imesema tume ya uchaguzi haina haki ya kumsimamisha Bwana Atiku kuwania Urais wa nchini humo.

Katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa majimbo uliofanyika jumamosi iliyopita ,chama tawala cha PDP kimeongoza kwa kuchukua majimbo 26 kati ya 32 .

Hadi hivi sasa matokeo hayo yanaonyesha chama cha upinzani cha ANPP kupata ushindi mkubwa katika majimbo ya kaskazini ya Bauchi, Borno, Yobe na Zamfara.

Chama cha Bwana Atiku cha Action Congress kimelitwaa jimbo la Lagos ilhali chama cha PPA kikijinyakulia jimbo la kusini mashariki la Abia.

Hapo awali kumeripotiwa machafuko kadhaa nchini humo ambapo jumla ya watu 21 wameuawa katika mapambano na polisi ,wakipinga matokeo hayo .

ABDIJAN-Eneo la mpaka kuondoshwa

Eneo lilokuwa likigawanya pande mbili za kijeshi nchini Ivory Coast huenda likaondolewa kufuatia makubaliano ya hivi karibuni kati ya waasi na serikali nchini humo.

Eneo hilo lenye urefu wa kilometa 600 lililokuwa chini ya uangalizi wa majeshi ya umoja wa mataifa na Ufaransa litakuwa huru baada ya majeshi hayo kuondoka katika vituo 17 vya uangalizi wiki chache zijazo.

Hiyo itakuwa ni hatua kubwa katika juhudi za kuliunganisha taifa hilo ambalo lilikumbwa na machafuko miaka kadhaa iliyopita .

Hivi karibuni serikali nchini humo ilitekeleza moja ya vipengele muhimu katika makubaliano ya mkataba wa amani baada ya Rais Laurent Bagbo kumteua kiongozi wa waasi Giume Sorro kuwa Waziri mkuu.

 • Tarehe 16.04.2007
 • Mwandishi Charles Mwebeya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CBHQ
 • Tarehe 16.04.2007
 • Mwandishi Charles Mwebeya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CBHQ

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com