1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

18 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CBHP

NEW YORK-Umoja wa mataifa wataka nchi jirani kusaidia wakimbizi wa Iraq

Umoja wa mataifa umetoa wito kwa nchi jirani na Iraq kufungua milango kwa ajili ya maelfu ya wakimbizi wanaokimbia machafuko nchini humo.

Akizungumza kwa njia ya video katika mkutano juu ya kuwasaidia maelfu ya wakimbizi kutoka Iraq uliondaliwa na shirika la wakimbizi duniani, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amezitaka pia nchi nyingine nje ya mashariki ya kati kusaidia tatizo hilo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya maofisa 450 kutoka nchi 60.

Kwa mujibu wa UNHCR , karibu wakimbizi milioni 2 kutoka Iraq wako katika nchi za mashariki ya kati wakijaribu kuokoa maisha yao kutokana na ghasia nchini mwao.

Taarifa hiyo ya UNHCR , imeongeza kuwa nchini Iraq kweyewe kuna idadi ya watu milioni 2 ambao hawana makazi.

Serikali ya Iraq imesema itatumia Euro milioni 18 kusaidia raia wake waliokimbilia nchi jirani.

TEHRAN-Raia wawili wa Sweden waachiwa huru Iran.

Iran imewaachia huru raia wawili wa Sweden waliokuwa gerezani nchini humo kwa makosa ya kufanya ujasusi.

Raia hao Stefan Johanson na Jari Hojmar ambao walikuwa wakifanya kazi katika kampuni moja ya ujenzi, wamekaa gerezani nchini Iran kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Watu hao wanadai walikamatwa wakati wakiwa wanachukua picha za kitalii na kuangalia wanyama aina ya Dolphin, mwezi January mwaka 2005.

Kwa mujibu wa maafisa wa Iran Raia hao walisamehewa na kuachiwa huru mapema wiki hii kwa nia njema.

Hivi karibuni Iran iliwaachia wanajeshi 15 wa jeshi la wanamaji wa Uingereza baada ya meli waliyokuwamo kukamatwa katika sehemu ya bahari ya nchi hiyo.

NaGASAKI-Meya wa Nagasaki auawa

Polisi nchini Japan imesema Meya wa mji wa Nagasaki Itcho Ito ameuawa kwa kupigwa risasi katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa serikali za miji karibu na kituo kikuu cha reli.

Muuaji ambaye anahusishwa na matukio kadhaa ya uhalifu alikamatwa mara baada ya tukio hilo akiwa na bastola ,ingawa hakuweka bayana sababu ya kufanya mauaji hayo.

Meya Ito aliyekuwa na umri wa miaka 61alikuwa akifanya mkutano wa kampeni akigombea tena nafasi hiyo, kwa muhula wa nne.

Alijipatia umaarufu mkubwa mjini humo kwa tabia yake ya kusema ukweli na kushika wadhifa huo kwa muda wa vipindi ´vitatu.

Alianza kushika wadhifa huo mwaka 1990 , baada ya aliyekuwa meya wa mji huo naye kupigwa risasi na mtu aliyetambulika kama mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.

ANKARA-Uturuki kufanya mabadiliko ya sheria

Uturuki imesema imedhamiria kufanya mabadiliko ya sheria zake ifikapo mwaka 2013 ili kufanikisha ombi lake la kujiunga na umoja wa nchi za ulaya .

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Abdullah Gul baada ya kuzindua mpango wa mabadiliko ya sheria inayohusisha mtiririko wa mazingira na nishati , viwanda pamoja na ushindani.

Mjini Brussels makao makuu ya nchi za umoja wa ulaya , Umoja wa huo umesifia hatua hiyo, lakini haukusema ni lini utafanya tahmini kwa kutegemea na maendeleo ya mabadiliko hayo nchini humo.

DACCA-Mtoto wa Kahled Zia aachiwa

Idara ya usalama nchini Bangladesh imemuachia mtoto wa aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Bibi Khaleda Zia.

Mtoto huyo bwana Arafat Rahman alikamatwa na majeshi ya Bangladesh mapema wiki hii.

Kuna taarifa kwamba kuachiwa kwake ni sehemu ya mapatano yaliyofikiwa baina ya serikali na Waziri mkuu huyo wa zamani.

Kwa mujibu wa mapatano hayo, bibi Khaled Zia ataruhusiwa kuondoka nchini humo na kwenda kuishi katika hifadhi ya kisiasa nchini Saudi Arabia.

BERLIN-Merkel atoa hakikisho Afrika kupewa kipaumbele

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amemuhakikishia mwanamuziki maarufu BONO; Kuwa mustakabali wa Afrika utapewa kipaumbele katika mkutano wa viongozi wa nchi nane tajiri duniani utakaofanyika mwezi Juni nchini Ujerumani.

Kansela Merkel amesema hayo baada ya kukutana na mwanamuziki huyo ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya kijamii.

Bwana BONO amesema ana hakika kuwa Kansela Merkel atatekeleza yale aliyoahidi.

Ujerumani ni mwenyekiti wa sasa wa kundi la nchi nane tajiri pamoja na baraza la tume ya umoja wa ulaya.

NEW YORK-Baraza la usalama lajadili mabadiliko ya jhali ya hewa

Kwa mara ya kwanza katika historia yake ya miaka 60, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeanza mjadala rasmi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Akizungumza kwa niaba ya Uingereza, Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama, Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo bi Margreth Becket, amesema kuwa ugeugeu wa hali ya hewa unachochea migogoro kutokana na mashinikizo ya uhamiaji unaosababisha ushindani katika kutafuta rasilimali.

Akifafanua zaidi kuhusu hoja yake Bi Beckett ametolea mfano mgogoro wa Sudan, kuwa chanzo chake ni mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababisha ufinyu wa rasilimali.

Akichangia katika mjadala huo , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki Moon ameitaka jumuiya ya kimataifa ichukue hatua za pamoja katika kuepusha mashindano ya kugombea nishati.

Hata hivyo mkutano huo umegubikwa na utata huku baadhi ya nchi wanachama wakiongozwa na China pamoja na Russia , zikidai Baraza hilo halikuwa na wajibu wa kuzungumzia masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Lakini msimamo huo wa China na Russia ulipingwa na Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Bi Margreth Beckett ambaye alisisitiza kuwa migogoro mingi duniani inachangiwa na hali hiyo.

VIRGINIA-Gavana ataka uchunguzi zaidi.

Gavana wa jimbo la Virginia ametaka ufanyike uchunguzi wa haraka juu ya tukio la kuuawa kwa watu 33 katika chuo kikuu cha ufundi cha mjini humo.

Tamko la Gavana huyo Tim Kein, limekuja kufuatia malalamiko ya wanafunzi wa chuo hicho kwamba, utawala wa chuo haukufanya jitihada za kutoa taarifa chuoni hapo wakati muuaji alipokuwa akiendelea kutekeleza kitendo hicho.

Katika taarifa yake jana kwa vyombo vya habari Polisi ilisema mtu aliyefanya mauaji hayo ni Cho Seung Hui, ambaye naye alijiua baada ya kuwawua wanafunzi 31 na mhadhiri mmoja kutoka India.

Taarifa kutoka jeshi la Polisi nchini Marekani zinasema Hui ,alihamia nchini Marekani toka Korea ya Kusini pamoja na wazazi wake mwaka 1992 akiwa na umri wa miaka minane, na kwa mujibu wa watu wa karibu nae wanadai alikuwa ni mtu mkimya na asiyekuwa na tabia za ukorofi.

Rais George Bush aliwaongoza Maelfu ya watu waliofurika katika chuo hicho wakiwa na maua pamoja na mishumaa, katika ibada maalum ya maombolezo.

Rais Bush amesema kitendo hicho kimepokewa kwa huzuni kubwa na watu wote wa Marekani.

ABUJA-Wapinzani wataka uchaguzi uahirishwe

Vyama vya upinzani nchini Nigeria vimeitaka serikali nchini humo kusogeza mbele uchaguzi wa Urais wa jumamosi ijayo la sivyo vitasusia uchaguzi huo.

Katika taarifa ya pamoja ya vyama 18 , vyama hivyo vimetishia kususia uchaguzi wa jumamosi endapo madai yao kadhaa hayatatekelezwa.

Miongoni mwa madai hayo ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa majimbo uliofanyika wiki iliyopita na kuvunjwa kwa tume ya uchaguzi.

Wakati vyama vya upinzani vikionekana kukata tamaa kabla ya uchaguzi wa urais Jumamosi ijayo, machafuko kadhaa yameripotiwa kaskazini ya nchi hiyo hususani katika jimbo la Kano.

Hapo jana kundi kubwa la watu lijulikanalo kama Taleban , lilikivamia kituo cha Polisi na kuauwa askari 12, pamoja na mwanamke mmoja, mke wa mkuu wa kituo hicho.

Hata hivyo taarifa kutoka Polisi zinadai kundi hilo limelipiza kisasi baada ya Polisi kumuua Imam wa msikiti mmoja wakati akiendesha ibada.

Wagombea wawili wa upinzani Atiku Abubakar na Muhamad Buhari , wanatazamiwa kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa chama tawala cha Peoples Demokratik bwana Umar Musa Yar adua anayeungwa mkono na Rais anayemaliza muda wake Oleshegun Obasanjo.

MOGADISHU-machafuko yazuka tena Somalia

Watu wawili wameuawa kufuatia mapigano yaliyozuka upya katika mji mkuu wa Somalia , Mogadishu.

Mapigano hayo baina ya vikosi vya Ethiopia na wanamgambo wa kiislam ni ya kwanza kwa siku za hivi karibuni ,baada ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa na makundi ya koo .

Mapatano ya hivi karibuni yalitokana na mapigano makali ya mwezi jana ambapo jumla ya watu 1,000 waliuawa na 4000 wengine kujeruhiwa.

Majeshi ya Ethiopia yako nchini Somalia toka January mwaka huu, baada ya kuisaidia serikali ya mpito nchini humo ,kuwaondosha wanamgambo wa kiislam.

Askari 1,500 wa jeshi la amani la umoja wa Afrika wapo nchini humo, ilhali Umoja huo ukiwa na mpango wa kuongeza askari wengine 6,500.