1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

30 Aprili 2007

Berlin-Wahimiza hatua zaidi kuchuliwa juu ya mgogoro wa Darfur

https://p.dw.com/p/CBHO

Mzozo wa Darfur umetimiza miaka minne huku Maandamano ya kutaka hatua zaidi kuchukuliwa juu ya mzozo wa huo ,yakifanyika sehemu mbalimbali duniani.

Siku ya kimataifa ya Mzozo wa Darfur iliandaliwa kwa pamoja na mashirika ya Haki za binaadam ya Amnesty International na Human Rights Watch.

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa takribani watu laki 2 wamepoteza maisha, na wengine zaidi ya milioni 2 wakiwa hawana makazi kutokana na mapigano yanayoendelea katika jimbo hilo la magharibi la Sudan.

Maandamano hayo yalifanyika katika miji ya Berlin, New York ,London, Cairo na Abuja.

Mchambuzi wa masuala ya Afrika Ulrich Deus, alishiriki katika maandamano mjini Berlin.

Serikali ya Sudan chini ya uongozi wa Rais Hassan Omar Al Bashir , unashutumiwa kwa kuliunga mkono kundi la Janjaweed , linalodaiwa kufanya mauaji dhidi ya watu wasio na hatia katika eneo hilo.

CAIRO-Iran kuhudhuria mjadala wa amani Iraq

Irani imesema itashiriki katika mkutano utakaozungumzia hali ya kisiasa na usalama nchini Iraq.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri Mohamad Ali Husseinkupitia katika televisheni ya taifa ya nchi hiyo, amesema ujumbe wa Iran utaongozwa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Manoucher Mottaki.

Mkutano huo unatazamiwa kufanyika katika mji wa kitalii wa Sherm El Sheikh nchini Misri, mwishoni mwa wiki hii.

Kauli hiyo imetolewa muda mfupi baada ya msafara wa Iran kuwasili mjini Baghdad kwa mkutano wa siku tatu na viongozi Iraq.

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleeza Rice, ambaye pia anatazamiwa kuhudhuria mkutano huo wa Sherm El Sheikh , hakuweka bayana iwapo atafanya mazungumzo na ujumbe wa Iran.

Akizungumza kwa njia ya Televisheni Bi Rice amesema mkutano wowote na waziri wa mambo ya nje wa Iran , Bwana Manoucher Mottaki ,tazungumzia masuala ya Iraq, na siyo uhusiano baina ya Marekani na Iran.

BERLIN-Bi Merkel ziarani Marekani

Kansela wa Ujerumani bi. Angela Merkel ambaye pia ni mwenyekiti wa nchi za Umoja wa ulaya ameelekea nchini Marekani ambapo anatazamiwa kuwa na mazungumzo na rais George Bush .

Viongozi hao wawili wanatazamiwa kusaini makubaliano yenye lengo la kuboresha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Umoja wa ulaya na Marekani.

Juhudi za kuzuia kuongezeka kwa hali ya joto duniani na masuala ya amani katika Kosovo na Afghanstan ni moja wapo ya agenda zitakazojadiliwa.

Haikuwekwa wazi endapo viongozi hao watazungumzia mpango tata wa Marekani wa kuweka mitambo ya usalama katika nchi za Poland na Jamhuri ya Czech.

INSTABUL-wataka tofauti , dini na siasa

Mamia ya maelfu ya watu wameingia mitaani mjini Instabul nchini Uturuki kuunga mkono juhudi za kutenganisha dini na siasa.

Waandamanaji wakiwa na mabango huku walisikika wakipaza sauti kukishutumu chama tawala kilichoweka mizizi katika dini ya kiislam.

Waandamanaji wanahofia kuwa endapo mgombea wa chama tawala atachaguliwa kama Rais, anaweza kulibadili taifa hilo kuwa la kiislam.

Chama tawala ambacho kina sauti kubwa katika bunge la nchi hiyo , kimetoa mgombea pekee bwana Mohamed Gul, ambaye ni waziri wa mambo ya nje .

Upinzani ndani ya bunge, ulipinga uchaguzi wa duru ya kwanza ijumaa iliyopita , ambapo Gul alishindwa kupata uungwaji mkono, kushinda uchaguzi huo.

BAMAKO-Matokeo ya uchaguzi yasubiriwa

Matokeo ya uchaguzi Mkuu nchini Mali yasubiriwa kuanza kutolewa huku Rais Amadou Toumani Toure akitazamiwa kupata ushindi .

Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi huo wamesema mchakato wa upigaji kura ulienda uzuri bila ghasia zozote.

Rais Toure ambaye aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi mwaka 1991, aliirudisha nchi hiyo katika utawala wa kiraia na kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2002.

Kiti cha Rais kinagombewa na watu saba , akiwemo Spika wa Bunge na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Ibrahim Boubakar Keita.

KABUL-Majeshi ya Muungano yaua Watalebani

Majeshi ya muungano ya muungano na Marekani yameripotiwa kuwaua waasi zaidi ya´100 wa kundi la Taleban, katika mapigano makali mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Muungano wa majeshi hayo, takribani wanamgambo 140 wa kundi la Taleban waliuawa katika mapigano tofauti,katika jimbo la magharibi la Herat.

Imeelezwa kuwa askari mmoja wa vikosi vya muungao aliuawa katika Mapigano hayo makali yaliyotokea katika bonde la Zerkoh.

Jimbo la Herat ambalo linapakana na Iran , limekuwa katika misukosuko mikubwa ya mapigano katika siku za hivi karibuni kati ya Wafuasi wa kundi la Taleban na vikosi vya majeshi ya Muungano.