1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

[No title]

9 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBHL

PARIS-Ufaransa yatoa tahadhari juu ya Wolfowitz

Ufaransa imetoa mwito wa kikao muhimu cha bodi ya wakurugenzi wa benki ya dunia kuamua kwa umakini hatma ya Rais wa Benki hiyo Paul Wolfowitz.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ufaransa Jean Baptiste Mattei , amesema nchi yake inataka bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo ,kulichukulia suala hilo kwa umakini mkubwa .

Kwa mujibu wa Bodi ya benki ya dunia , Bwana Wolfowitz amepatikana na makosa kadhaa ya kiutendaji, ikiwamo kumpandisha cheo mpenzi wake kinyume na utaratibu wa benki hiyo.

Hii leo Ujerumani imemtaka mwakilishi wa benki hiyo nchini mwake , kuunga mkono mapendekezo ya kumtakaBwana Wolfowitz kujiuzulu.

Mkutano wa bodi ya Benki hiyo ndio utakaoamua Hatma ya Mkuu huyo wa benki ya Dunia mapema wiki hii.

RIYADH-Mmoja anyongwa Saudi Arabia

Mwanamke mmoja raia wa Ethiopia amehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa , baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.

Khadija Ibrahim Musa alipatikana na hatia ya kumuua Mohamed Abdullah Kamal Shaeen ambaye ni raia wa Misri, kwa kumvunja shingo wakati mwanaume huyo alipokuwa amelala.

Khadija anakuwa ni mtu wa 58 kunyongwa na serikali ya Saudi Arabia mwaka huu.

Adhabu ya kifo kutokana na makosa ya ubakaji , mauaji,ujambazi , madawa ya kulevya na uhaini, imekuwa ikifanywa hadharani nchini Saudi Arabia, kwa mujibu wa sheria za dini ya kiislam.

MOGADISHU- Mavazi ya wanawake yapigwa marufuku Somalia

Vikosi vya usalama nchini Somalia vinatuhumiwa kunyang’anya na kisha kuchoma moto nguo zinazovaliwa na wanawake ,ili kuwagundua wapiganaji wa kiislam wanaotumia mavazi hayo kujikinga na mashambulizi.

Mavazi hayo yanayofunika mwili wote pamoja na kubakiza sehemu ya macho pekee , huvaliwa na asilimia kubwa ya wanawake mjini Mogadishu, hususani katika kipindi cha utawala wa muungano wa mahakama za kiislam .

Akizungumzia juu ya shutuma hizo , msemaji wa Polisi Ali Nur, amesema wapiganaji waliosalia wa kiislam mjini Mogadishu, wamekuwa wakitumia mavazi hayo kufanya mashambulizi ya kushtukiza ,ama kujificha dhidi ya vikosi vya usalama.

BERLIN-Ulinzi waimarishwa mkutano G8

Ujerumani imeweka ulinzi mkali dhidi ya vitendo vya kigaidi katika miji sita ya kaskazini ya nchi hiyo, katika maandalizi ya mkutano wa G8 , unaotazamiwa kuanza mwezi ujao mjini Hailigen-Dam.

Jeshi la Polisi limesema limehakikisha ulinzi wa kutosha katika miji hiyo ya kaskazini ya Ujerumani kufuatia hofu ya shambulio la kigaidi .

Kufuatia hali hiyo Polisi imeamuru kufunga vituo kadhaa vya kitamaduni katika miji ya Hamburg na Berlin.

Wahusika kadhaa wa shambulio la September 11, mwaka 2001 nchini Marekani , walikuwa wakaazi wa mji wa Hamburg.

DILI- Uchaguzi Timor Mashariki wamalizika kwa amani

Uchaguzi wa duru ya pili wa Urais Timor ya mashariki umemalizika huku mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Hosee Ramos Horta akitazamiwa kumshinda kiongozi wa waasi wa zamani Franswaar Guteres .

Huo utakuwa uchaguzi wa kwanza wa Timor ya Mashariki , taifa lililopata uhuru wake mwaka 2002 kutoka Indonesia.

Matokeo kamili ya uchaguzi huo yanatazamiwa kutangazwa keshokutwa.

Mapema kabla ya uchaguzi huo Rais anayemaliza muda wake Shanana Gushmao, aliwataka wananchi wa Timor ya mashariki kufanya uchaguzi kwa amani.

Ripoti zinasema uchaguzi huo umefanyika kwa amani bila ya ghasia zozote.

BAGHDAD-Marekani , Iraq kufanya kazi pamoja kuleta amani

Marekani na Iraq zimesema zitaendelea kufanya kazi pamoja kuleta amani nchini Iraq.

Makamu wa Rais wa Marekani Dick Cheney pamoja na Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri Al Malik wamesema nchi hizo zinaguswa na machafuko yanayotokea nchini humo .

Malik ambaye amekuwa akishinikizwa na Washington kufanya jitihada za haraka kupunguza ghasia nchini humo, ameiomba Marekani kuendelea kuipa ushirikiano nchi yake hususani katika masuala ya ulinzi na usalama.

Akizungumza kwa upande wake katika mkutano na waandishi wa habari , makamu huyo wa Rais wa Marekani amesema lengo la kwenda nchini Iraq , ni jitihada za Marekani kujaribu kuishawishi serikali ya Iraq kuandaa mazunguzo na vikundi vya kidini vinavyosababisha machafuko na vifo kila uchao.

Mchana wa leo waandishi wanne wa habari wameripotiwa kuuawa katika mji wa Kirkuk.

Waandishi hao kabla ya kuuawa , waliteswa na kisha kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

LONDON-Wanne wanaswa shambulio la London.

Watu wanne akiwemo mjane wa kinara wa shambulio la kujitoa mhanga la mjini London , mwezi Julai mwaka 2005 wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo.

Watu hao wanne wanatuhumiwa kula njama za kupanga na kuandaa vitendo vya kigaidi.

Askari wa usalama wa Uingereza waliwakama washukiwa hao baada ya msako mkali leo asubuhi katika miji ya Yorkshire na Midlands.

Washukiwa hao wamesafirishwa mjini London kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.

Mlipuko wa bomu la kujitoa mhanga , mnamo mwaka 2005 mjini London , ulipoteza maisha ya watu 52 na kujeruhi zaidi ya watu 700.

MANILA-wanane wauawa Filipino

Vikosi vya usalama katika mji mkuu wa Ufilipino , Manila , viko katika tahadhari kubwa kufuatia mlipuko wa bomu ulioua watu wanane.

Mlipuko huo wa bomu unaoaminiwa kufanywa na kundi la wapiganaji wa kiislam umetokea katika soko moja katika mji wa kusini wa Tacurong.

Mamia ya watu wamejeruhiwa kufuatia mlipuko huo.

Maafisa wa usalama wanasema huenda wanalishutumu kundi la Jamaa Islamiyah kuhusika katika shambulizi hilo.